Asasi za Kiraia Zasisitiza Kusitishwa kwa Mapigano Mashariki mwa DRC

international | Sun Feb 09 2025


Asasi za Kiraia Zasisitiza Kusitishwa kwa Mapigano Mashariki mwa DRC

Jukwaa la Kitaifa la Asasi za Kiraia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Kanda wa Jukwaa la Asasi za Kiraia za Nchi za Maziwa Makuu, limetoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano yanayoendelea mashariki mwa DRC, likionya kuwa vurugu hizo zinaathiri utulivu wa kanda nzima.


Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mjumbe wa Jukwaa hilo, Kennedy Walusalo, alisema kuwa asasi hizo zinaunga mkono maazimio yaliyotolewa na mkutano wa dharura wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Mkutano huo uliofanyika mwishoni mwa wiki, ulitangaza hatua 13 za kisheria na kiusalama kwa lengo la kumaliza mgogoro huo.


Walusalo alifafanua kuwa asasi za kiraia zilizokutana jijini Dar es Salaam kuanzia Februari 7 hadi 9, mwaka huu, zimekubaliana kwa kauli moja kuunga mkono juhudi hizo za kutafuta amani na suluhisho la kudumu.


"Kuongezeka kwa ukosefu wa usalama mashariki mwa DRC ni tishio kubwa kwa kanda nzima. Ikiwa mgogoro huu hautashughulikiwa kwa haraka, hali inaweza kuwa mbaya zaidi na kuhatarisha utulivu wa eneo la Maziwa Makuu," alisema Walusalo.


Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Emily Kariuki, aliungana na wadau wengine wa asasi za kiraia kusisitiza haja ya juhudi za pamoja za kanda kuhakikisha suluhisho shirikishi linapatikana.


Katika maazimio yao, wadau hao walitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja na kuondolewa kwa vikosi vya kigeni vilivyopo katika DRC bila mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo.


Aidha, asasi hizo zilitaka haki itendeke kwa waathiriwa wa machafuko, huku zikisisitiza umuhimu wa kuunganisha mchakato wa mazungumzo ya Luanda na Nairobi ili kuimarisha majadiliano kati ya DRC na Rwanda.


"Washiriki walisisitiza umuhimu wa kuwepo mtazamo wa pamoja wa kanda katika kushughulikia changamoto za kiusalama, kibinadamu, na kisiasa zinazolikumba eneo la Maziwa Makuu," alieleza Walusalo.


Alihitimisha kwa kutoa pongezi kwa wakuu wa nchi za kanda kwa kuandaa mkutano huo muhimu, akisema ulikuwa hatua inayokuja kwa wakati muafaka ili kujadili hali ya usalama katika DRC na kutoa suluhisho madhubuti.

I recommend this article.

You can participate in article recommendations up to 50 times within 24 hours.


0 comments


Messages unrelated about this certain topic may be deleted or restricted.

0/300
Loading...

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.