DRC: Juhudi za Amani Zagubikwa na Waasi, ADF Watikisa Kaskazini Mashariki

economy | Wed Jul 30 2025


DRC: Juhudi za Amani Zagubikwa na Waasi, ADF Watikisa Kaskazini Mashariki

Hali ya amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inaendelea kuwa tete, licha ya kuwepo kwa juhudi kubwa za usuluhishi kutoka pande mbalimbali za kimataifa. Takribani makundi 100 ya waasi, likiwemo kundi la M23 na lile hatari la ADF, yanaendelea kuleta machafuko na athari kubwa za kijamii na kiusalama nchini humo.


Wiki iliyopita, taarifa za kusikitisha zilitikisa ulimwengu baada ya mashambulizi mabaya yaliyofanywa na waasi wa ADF kaskazini mashariki mwa DRC kusababisha vifo vya watu zaidi ya 40. Vyombo vya habari vya kimataifa vilieleza kuwa tukio hilo lililothibitishwa na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO) na Jeshi la DRC, lilitokea kwenye nyumba ya ibada Jumapili iliyopita, na kusababisha hofu kubwa kwa wananchi.


Mwezi Machi mwaka huu, kulifanyika mkutano muhimu kati ya Waziri wa Nchi wa Qatar, Mohammed Al-Khulaifi, na Massad Boulos, Mshauri Mkuu mpya wa Ikulu ya White House kwa Afrika. Mkutano huo ulikuwa sehemu ya juhudi za pamoja za kutafuta suluhisho la kudumu la mizozo inayoendelea katika ukanda wa Maziwa Makuu. Japokuwa kulionekana dalili chanya katika mazungumzo kati ya kundi la AFC/M23 na wajumbe kutoka Ofisi ya Rais wa DRC yaliyofanyika jijini Doha, bado hakuna makubaliano rasmi ya kusitisha mapigano. Pande hizo mbili zilitangaza tu nia yao ya kufanya kazi pamoja kuelekea makubaliano kamili ya amani, lakini si makubaliano kamili ya kusitisha vita.


Asili na Vitendo vya Waasi wa ADF

Eneo la mashariki mwa DRC limekuwa ngome ya waasi kwa muda mrefu, na migogoro hii mara nyingi huenea hadi nchi jirani kama Rwanda, Burundi, na Uganda. Kati ya makundi hatari zaidi yanayotikisa ukanda huo ni Allied Democratic Forces (ADF), kundi la Kiislamu lililoundwa nchini Uganda miaka ya 1990. Hapo awali, ADF lilijihusisha na migogoro ya ndani nchini Uganda, likidaiwa kuwa na malengo ya kuondoa serikali ya Rais Yoweri Museveni, wakidai unyanyasaji dhidi ya Waislamu.


Baada ya kushindwa na Jeshi la Uganda mwaka 2001, ADF walihamia Mkoa wa Kivu Kaskazini nchini DRC. Ingawa kulikuwa na kipindi cha utulivu, kundi hilo liliibuka tena mwaka 2014, likianza kuratibu mashambulizi dhidi ya raia wasio na hatia nchini DRC. Musa Seka Baluku alichukua uongozi wa kundi hilo mwaka 2015 baada ya mtangulizi wake, Jamil Mukulu, kukamatwa. Baluku anaripotiwa kutangaza utii wake kwa kundi la kigaidi la Islamic State (IS) tangu mwaka 2016.


Ni hadi Aprili 2019, ndipo IS walikiri rasmi kuendesha shughuli zao katika eneo hilo, wakidai kuhusika na mashambulizi dhidi ya vituo vya jeshi karibu na mpaka wa Uganda. Taarifa hiyo ilitangaza kuanzishwa kwa IS Central Africa Province (ISCAP), ambayo baadaye ilijumuisha hata nchi ya Msumbiji. Ingawa kuna dalili za wazi za ushirikiano kati ya IS na ADF, IS haijalitambua waziwazi kundi la ADF katika matangazo yao ya propaganda. Septemba 2020, Baluku hata alidai kuwa ADF haipo tena, akisema, "Kwa sasa sisi ni mkoa, mkoa wa Afrika ya Kati, ambao ni mmoja wa mikoa mingi inayounda Islamic State."


Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limeripoti kuwa ADF wamewaua mamia ya raia na kuwalazimisha zaidi ya watu 40,000 kuhama kutoka eneo la Beni pekee tangu Januari 2021. Kundi hili la waasi pia linawalenga wanajeshi wa serikali na wale wa Umoja wa Mataifa, na tangu IS iibuke nchini DRC, mashambulizi yameongezeka kwa kasi. Mashambulizi ya ISCAP hutokea katika maeneo yanayodhibitiwa na ADF, hususan Kivu Kaskazini katika eneo la Beni, na wakati mwingine huenea hadi mkoa jirani wa Ituri. Mashambulizi haya mara nyingi hulenga kambi za jeshi, lakini pia yamefanywa dhidi ya Wakristo, huku tukio kubwa zaidi likitajwa kuwa la Oktoba 2020 kwenye gereza la Beni, lililosababisha zaidi ya wafungwa 1,000 kutoroka.


Mazungumzo ya Amani na Uhusiano wa Kikanda

Mwezi Machi mwaka huu, Rais wa DRC, Felix Tshisekedi, na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame, walikutana nchini Qatar kwa mazungumzo yao ya kwanza ya ana kwa ana tangu kundi la M23 lilipoanza mashambulizi mashariki mwa Kongo mwezi Januari. Mkutano huu, ulioongozwa na Amir wa Qatar, ulikuja siku moja tu baada ya kundi la M23 kujiondoa kwenye mazungumzo mengine yaliyofanyika Angola, ikiwa tayari imeteka miji miwili mikubwa mashariki mwa Kongo.


Congo inaendelea kuishutumu Rwanda kwa kuwapa silaha na kuwaunga mkono waasi wa M23, ambao mashambulizi yao yameitumbukiza mashariki mwa Kongo katika mzozo mbaya zaidi katika miongo kadhaa. Kwa upande wake, Rwanda imekana madai hayo, ikisisitiza kuwa vikosi vyake vinafanya kazi ya kujilinda dhidi ya jeshi la Kongo na wanamgambo wanaoshambulia Kigali. Hali hii ya kutoaminiana inaendelea kuzorotesha juhudi za amani na kuongeza ugumu wa kutafuta suluhisho la kudumu la mzozo huu unaoendelea kuhatarisha maisha ya mamilioni ya watu nchini DRC na ukanda mzima wa Maziwa Makuu.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.