Wanawake na watoto wametajwa kuwa wahanga wakuu wa athari za kiafya na kimazingira zinazotokana na shughuli za uchimbaji mdogo wa madini nchini, huku matumizi ya kemikali hatari ya zebaki yakitajwa kuwa chanzo kikuu cha janga hilo. Haya yamebainika katika mjadala maalum ulioandaliwa na Shirika la HakiRasilimali jijini Dar es Salaam, uliowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo.
Akifungua mjadala, Msaidizi wa Mikakati na Ushirikiano kutoka HakiRasilimali, Irene Mosha, alieleza kuwa tafiti zinaonyesha hali ni mbaya, kwani takriban migodi 197 ya wachimbaji wadogo nchini bado inategemea zebaki katika kuchenjua dhahabu. Cha kutisha zaidi, alisema asilimia 71 ya maeneo hayo ya uchimbaji yamezungukwa na makazi ya watu, jambo linaloweka jamii nzima, hasa watoto na wanawake ambao hutumia muda mwingi nyumbani, katika hatari kubwa ya kiafya.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Katibu wa Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA), Salma Kundi, aliyefafanua kuwa wanawake wako katika hatari zaidi kwa sababu ya majukumu yao ya kifamilia na ukosefu wa mitaji. Alisema wengi wao hulazimika kufanya kazi katika mazingira hatarishi na kushika kemikali hiyo bila vifaa vya kujikinga ili kujipatia kipato cha kuhudumia familia.
Kwa upande wa serikali, Naibu Kamishna wa Madini anayeshughulikia Uwezeshaji na Uwajibikaji kwa Jamii, Terence Ngole, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kueleza mipango ya Wizara ya Madini kukabiliana nayo. Alisema wizara inatekeleza programu endelevu za kuwahamasisha na kuwapa wachimbaji wadogo teknolojia mbadala ili waachane kabisa na matumizi ya zebaki.
“Tunafahamu madhara ya zebaki na tunajitahidi kuwapa elimu wachimbaji kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMIKO) na kuwatengenezea mazingira wezeshi, ikiwemo kuwapa leseni za pamoja ili shughuli zao ziwe rasmi na salama,” alisema Ngole. Aliongeza kuwa, ingawa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 inazuia uchimbaji na uuzaji bila leseni, serikali hutumia busara kuruhusu mwananchi aliyeokota madini kwa bahati shambani kwake kuuza baada ya mamlaka kujiridhisha.
Kuhusu ajali za mara kwa mara migodini, Ngole alisema nyingi zinasababishwa na uzembe, kutofuata sheria za usalama, pamoja na athari za kimazingira kama mvua kubwa. Alisema wizara imeongeza idadi ya taasisi za usimamizi ili kuhakikisha usalama na afya vinazingatiwa katika maeneo yote ya uchimbaji nchini.