Mkoani Geita, ambako ardhi inatema dhahabu na maisha ya wengi yanategemea utajiri huo wa asili, kumeibuka tahadhari nzito inayolenga kuokoa maisha ya maelfu ya "Wana-Apolo" (wachimbaji wadogo). Hii ni kufuatia tishio la kimyakimya la kemikali ya Zebaki (Mercury), ambayo imekuwa ikitumika kwa miongo kadhaa katika uchenjuaji wa madini hayo, huku ikiacha madhara makubwa ya kiafya na kimazingira.
Katika kukabiliana na janga hilo, Taasisi isiyo ya kiserikali ya FADEV, ambayo imejikita katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo, imekuja na mkakati mpya wa kutoa elimu na vifaa kinga. Akizungumza wakati wa mafunzo maalum kwa wakufunzi na wawezeshaji mjini Geita juzi, Mratibu wa Programu kutoka FADEV, Bw. Martino Mbangile, amesisitiza kuwa utajiri wa dhahabu haupaswi kugharimu uhai wa mchimbaji.
Zebaki: 'Muuaji' Anayependwa na Wachimbaji Bw. Mbangile amebainisha kuwa licha ya madhara yake, Zebaki bado ni "shoka" la mchimbaji mdogo katika kutenganisha dhahabu na mchanga. Hata hivyo, amewataka wachimbaji hao kubadili mazoea kwa kuanza kutumia vifaa kinga (PPE) wakati wote wanapochanganya kemikali hiyo.
"Tunatoa elimu hii ili kupunguza athari za zebaki. Tunafahamu kuwa kutotumia kabisa zebaki kwa sasa ni mtihani mgumu maana ndio tegemeo kuu la wachimbaji wadogo kiuchumi. Lakini tunataka wapunguze madhara; wavae 'glovs' (mipira ya mikono) na mabuti (gumboots) ili hata kemikali ikimwagika isiwaguse ngozi moja kwa moja," alisisitiza Mbangile.
Aliongeza kuwa kemikali hiyo ina tabia ya kuingia mwilini kupitia ngozi au mvuke na kusababisha madhara ya kudumu kwenye mfumo wa fahamu, figo, na hata kuathiri vizazi vijavyo. Athari hizi hazichagui; zinawapata watu wazima, wajawazito, watoto, na hata mifugo inayokunywa maji yaliyochafuliwa na uchenjuaji huo.
Matumaini Mapya: Teknolojia ya 'Kigida' Wakati dunia ikipiga vita matumizi ya Zebaki kupitia Mkataba wa Minamata ambao Tanzania iliridhia, wataalamu wanaendelea kuumiza kichwa kutafuta mbadala. Bw. Mbangile amefichua kuwa kuna teknolojia mpya inayoitwa "Kigida" ambayo ipo katika hatua za majaribio ya kiutafiti.
"Teknolojia hii ya Kigida inatumika katika hatua ya mwisho ya ukamatishaji wa dhahabu. Ijapokuwa bado haijathibitishwa kutoa tija kamili kibiashara, tuna imani kubwa kuwa ndiyo itakuwa mkombozi wetu hapo baadaye na kupunguza matumizi ya zebaki migodini," alifafanua.
Serikali na Uhaba wa Zebaki Sokoni Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Geita (GEREMA), Bw. Misana Jeremiah, amekiri kuwa hali imebadilika. Amesema kuwa hatua ya serikali kusaini mikataba ya kimataifa ya kudhibiti zebaki imesababisha kemikali hiyo kuanza kuadimika sokoni na bei kupanda, jambo linalowashinikiza wachimbaji kutafuta njia mbadala na salama zaidi.
"Serikali inafanya jitihada za makusudi ili tuachane na kemikali hii hatari. Uhaba wake sokoni ni ishara tosha kuwa tunapaswa kubadilika," alisema Misana.
Mbali na kutoa "shule" hiyo ya darasani, FADEV haikuishia maneno matupu; imegawa vifaa kinga mbalimbali kwa wachimbaji hao, lengo likiwa ni kuwawezesha kufanya kazi katika mazingira salama na rafiki wa mazingira.
Tanzania ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa dhahabu barani Afrika, huku wachimbaji wadogo wakichangia sehemu kubwa ya pato la taifa na ajira. Hata hivyo, matumizi ya zebaki yamekuwa changamoto kuu inayohitaji ushirikiano wa dhati kati ya serikali, wadau wa maendeleo, na wachimbaji wenyewe ili kufikia uchimbaji endelevu.