Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametoa agizo kali kwa wakuu wa kampuni za Kichina zinazojenga barabara za mwendokasi jijini Dar es Salaam kufika nchini haraka iwezekanavyo kwa mazungumzo na serikali, ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa kasi inayotakiwa. Agizo hili linatokana na wasiwasi mkubwa alionao juu ya ucheleweshaji wa utekelezaji wa ujenzi huo, licha ya fedha za miradi kuwa tayari zimetolewa na serikali.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo, Waziri Ulega alibainisha kuwa moja ya changamoto kubwa inayokwamisha kasi ya ujenzi ni kucheleweshwa kwa uhamishaji wa fedha kutoka China, kwani akaunti za kampuni husika ziko nje ya Tanzania. Hii inasababisha ucheleweshaji wa manunuzi ya vifaa na malipo ya wafanyakazi, na hivyo kuathiri ratiba ya ujenzi.
"Barabara hizi tunazijenga kwa mikopo, na tunapofika muda wa kurejesha mkopo, tunapaswa kulipa hata kama miradi haijakamilika. Hili ni mzigo kwa wananchi mara mbili. Wakandarasi wanapaswa kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa," alisisitiza Waziri Ulega.
Aliongeza kuwa atashirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ili kuhakikisha viongozi wa kampuni hizo wanawasili nchini na kutoa maelezo juu ya ucheleweshaji huo. "China ni marafiki wa dhati wa Tanzania, na kwa sababu hiyo ni muhimu kuambiana ukweli na kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote," alisema.
Miradi ya ujenzi wa barabara za mwendokasi jijini Dar es Salaam imekuwa ikisuasua licha ya fedha kuwepo. Barabara zinazohusika ni pamoja na Bagamoyo Maktaba – Mwenge, Mwenge - Tegeta, na Ubungo – Kimara. Katika ukaguzi wa barabara ya Ubungo – Kimara, Waziri Ulega alibaini kuwa kampuni ya Sichuan kutoka China haijaweka mtambo wa kutengeneza lami kama ilivyopaswa kwa mujibu wa mkataba. Pia, aliona kuwa baadhi ya maeneo ya ujenzi hayana wasimamizi rasmi wa mradi, jambo ambalo ni kinyume na makubaliano.
"Fedha zinazotolewa kwa miradi hii zinaweza kutumika katika maeneo mengine yenye uhitaji mkubwa. Rais Samia Suluhu Hassan ametenga fedha hizi kwa sababu anajua umuhimu wa miundombinu bora katika kukuza uchumi wa taifa," alisema Ulega.
Waziri alifichua kuwa kuna mradi uliopaswa kuwa umekamilika kwa zaidi ya asilimia 60, lakini hadi sasa umefikia asilimia 23 pekee. "Hili si jambo jema kwa taifa linalojijenga kiuchumi. Wananchi wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla wanahitaji barabara hizi zikamilike kwa wakati," alisisitiza.