VETA Gorowa ‘Yapika’ Jeshi la Vijana 800 Manyara, DC Kaganda Ataka Wasibweteke

economy | Sun Nov 23 2025


VETA Gorowa ‘Yapika’ Jeshi la Vijana 800 Manyara, DC Kaganda Ataka Wasibweteke

Katika hatua inayotajwa kama mapinduzi ya kimya kimya ya kiuchumi mkoani Manyara, Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) tawi la Gorowa, lililopo wilayani Babati, kimefanikiwa kuingiza sokoni 'jeshi' la nguvukazi yenye ujuzi wapatao 866. Hatua hii inatafsiriwa kama mwarobaini wa kudumu wa tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana waishio vijijini, ikiwa ni utekelezaji wa vitendo wa sera ya serikali ya kujenga uchumi wa viwanda kupitia rasilimali watu.


Akisoma taarifa ya kina wakati wa mahafali ya nne ya chuo hicho yaliyofanyika jana, Mkuu wa Chuo cha VETA Gorowa, Bw. Joshua Matagane, alijinasibu kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho Julai 2020, kimekuwa kimbilio la wakazi wa Babati na vitongoji vyake. Alibainisha kuwa mwamko wa wananchi umekuwa mkubwa, jambo lililopelekea wananchi 680 kunufaika na mafunzo ya muda mfupi (Short Courses).


"Tunaona mabadiliko makubwa sana kwenye mtazamo wa jamii. Katika kundi hili la mafunzo ya muda mfupi, tuna wanaume 511 na wanawake 169 ambao sasa wana ujuzi mkononi wa kuwasaidia kuendesha maisha yao bila kutegemea kuajiriwa ofisini," alisema Matagane.


Uzalishaji wa Wataalamu wa Muda Mrefu Mkuu huyo wa chuo aliendelea kufafanua kuwa, mbali na kozi fupi, chuo kimefanikiwa kutoa mafunzo ya muda mrefu kwa vijana 186 (wavulana 117 na wasichana 69) tangu kuanzishwa kwake. Katika mahafali ya mwaka huu pekee, chuo kimewatunuku vyeti wahitimu 38 walioiva katika fani mbalimbali, wakiwemo wanaume 21 na wanawake 17.


Kwa sasa, VETA Gorowa imekuwa 'lulu' kwa kutoa mafunzo katika fani zinazogusa mahitaji ya moja kwa moja ya jamii (demand-driven skills). Fani hizo ni pamoja na Umeme wa Majumbani, Ufundi Bomba, pamoja na Ushonaji wa Nguo na Ubunifu wa Mitindo. Matagane aliahidi kuwa uongozi wa chuo hautalala, na tayari wana mikakati ya kuongeza fani mpya katika mwaka ujao wa masomo ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na soko.


Rai ya Serikali: "Tokeni Mkafanye Kazi" Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Emmanuela Kaganda, alitumia jukwaa hilo kuwapa "nondo" wahitimu hao. Aliwataka kutobweteka na vyeti walivyopata, bali watumie ujuzi huo kama mtaji wa kujikomboa kifikra na kiuchumi.


"Serikali imewekeza fedha nyingi kuwaletea chuo hiki hapa kijijini. Ujuzi mlioupata leo usiwe pambo la ukutani. Tokeni hapa mkajiajiri na, ikiwezekana, muajiri na wengine. Hii ndiyo tafsiri sahihi ya kujitegemea," alisisitiza DC Kaganda.


Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuimarisha sera ya ufundi stadi kwa kuhakikisha vyuo vya VETA vinajengwa na kuboreshwa maeneo ya vijijini ili kupunguza wimbi la vijana kukimbilia mijini bila ujuzi.


Kilio cha Wahitimu Awali, akisoma risala kwa niaba ya wenzake, mhitimu Bi. Saumu Ally, aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuboresha miundombinu ya kujifunzia chuoni hapo. Ombi kuu la wanachuo hao lilikuwa ni ujenzi wa maktaba ya kisasa itakayowasaidia katika tafiti na kujisomea, pamoja na kuongezwa kwa fani nyingine ili kutoa wigo mpana wa machaguo kwa vijana wenye vipaji tofauti.


Mafanikio haya ya VETA Gorowa ni kielelezo tosha kuwa elimu ya ufundi inazidi kupewa kipaumbele na jamii ya Watanzania kama njia ya uhakika ya kupambana na umaskini.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.