Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limetoa onyo kali kwa watu na makundi yanayotumia mitandao ya kijamii kujinadi kuwa yanawezesha wananchi kiuchumi, huku ikibainika kuwa ni njama ya udanganyifu na wizi. Chombo hicho cha serikali kimesisitiza kuwa vitendo hivyo sasa ni kosa la jinai chini ya sheria iliyoboreshwa, na wahusika watakabiliwa na mkono wa sheria.
Akifafanua jijini Dar es Salaam, Mwanasheria wa NEEC, Emmanuel Kalengela, alieleza kuwa Sheria ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi, Sura ya 386, ambayo ilifanyiwa marekebisho na kupitishwa na Rais Samia Suluhu Hassan mwezi Machi 2025, imeweka meno makali kudhibiti wimbi hili la utapeli. "Sheria sasa inamlinda mwananchi dhidi ya upotoshaji. Mtu yeyote atakayebainika anatoa matangazo ya uongo ya uwezeshaji atachukuliwa hatua kali," alisema Kalengela. Alifafanua kuwa adhabu kwa kosa hilo ni kifungo cha mwaka mmoja jela au faini isiyopungua Shilingi laki tano (TZS 500,000) na isiyozidi Shilingi milioni hamsini (TZS 50,000,000).
Wakati onyo hilo likitolewa, Kaimu Katibu Mtendaji wa NEEC, Neema Mwakatobe, alifichua kuwa serikali kupitia baraza hilo imedhihirisha kwa vitendo dhamira yake ya kuwainua wananchi. Alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 pekee, NEEC imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi trilioni 2.44 kwa wanufaika takriban milioni 18 kote nchini. "Fedha hizi ni halisi na zimewafikia wananchi, ambapo asilimia 51 ni wanaume na asilimia 49 ni wanawake, kuonyesha dhamira yetu ya usawa," alisema Mwakatobe.
Aliongeza kuwa, NEEC imeamua kuwashirikisha waandishi wa habari kwa kuwapa mafunzo maalum ili wawe daraja la kupeleka taarifa sahihi kwa umma, na kuwaepusha na mitego ya matapeli. "Mwananchi hawezi kuwezeshwa bila taarifa sahihi. Kupitia vyombo vya habari, watu watajua wapi pa kwenda na nini cha kufanya wanapohitaji msaada wa kiuchumi," alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa NEEC, Gwakisa Bapala, alitoa takwimu zinazoonyesha umuhimu wa jitihada hizo, akisema hapo awali ni asilimia 10 tu ya Watanzania walikuwa wananufaika moja kwa moja na ukuaji wa uchumi kutokana na changamoto za mitaji na ujuzi. Hivyo, mikakati ya sasa inalenga kubadili hali hiyo na kuhakikisha maendeleo yanamgusa kila mwananchi.