Umuhimu wa usalama na uaminifu katika masuala ya kidijitali umeelezwa kuwa ndio msingi mkuu katika kujenga uchumi imara wa kidijitali nchini Tanzania. Hii ni kutokana na kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazohusiana na usalama wa kimtandao na ulinzi wa taarifa za siri za watumiaji wa mitandao, si tu nchini bali pia kimataifa.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA nchini (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga, alipokuwa akifungua rasmi Jukwaa la Nne la Usalama wa Kimtandao la Tanzania kwa mwaka 2025, lililofanyika jijini Arusha. Jukwaa hilo la siku mbili limekutanisha takribani washiriki 200 kutoka ndani na nje ya nchi.
Dkt. Mwasaga alisema kuwa Tanzania imeweka mkazo katika nguzo kuu tano ili kufanikisha mageuzi makubwa katika sekta ya kidijitali. Nguzo hizo ni pamoja na kukuza ujuzi wa kidijitali miongoni mwa wananchi, kuhakikisha usalama na uaminifu katika masuala yote ya kidijitali, kuimarisha huduma za mawasiliano ya kidijitali, kujenga uchumi imara wa kidijitali, na kufanya tafiti za kidijitali, ubunifu, na kukuza ujasiriamali katika sekta hii.
Alieleza kuwa kutokana na kuzingatia nguzo hizo tano, Tanzania imeanza kuona mabadiliko chanya katika masuala ya kidijitali na usalama wa kimtandao. Hii ni pamoja na wananchi kutumia na kunufaika na teknolojia pamoja na majukwaa mbalimbali ya kidijitali, hali ambayo inasaidia kuimarisha ushindani katika uchumi wa Tanzania.
"Nguzo ya usalama na uaminifu wa kidijitali ni muhimu sana. Hii ndio nguzo ambayo inazungumzia kuhusu ulinzi wa kimtandao na kuhakikisha taarifa binafsi za watu zinalindwa. Huu ndio msingi wa uaminifu tunapojenga uchumi wa kidijitali ambao unahusisha idadi kubwa ya watu," alisisitiza Dkt. Mwasaga.
Aliongeza kuwa, "Hivyo, jukwaa kama hili, ambalo linafanyika mara moja kwa mwaka, ni muhimu sana kwetu kwa sababu linatupa fursa ya kuwasikiliza wataalamu wetu wa TEHAMA kutoka ndani na nje ya nchi ili kujadili mambo ambayo ni ya msingi kwa maendeleo ya nchi yetu."
Dkt. Mwasaga alifafanua kuwa kwa mujibu wa ripoti ya kimataifa kuhusu masuala ya kimtandao (GCI) ya mwaka 2024, Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kwa kuorodheshwa katika Daraja la Kwanza miongoni mwa nchi 46 duniani zinazofanya vizuri katika masuala ya ulinzi wa kimtandao, ambayo ni nafasi ya juu kabisa duniani.
Kulingana na ripoti hiyo, alisema kuwa kila ukanda duniani una nchi ambazo ni mfano wa kuigwa au zinaendelea vizuri katika masuala haya, na pia kila ukanda una nchi ambazo ziko katika hatua za mwanzo za kujenga mifumo imara ya usalama wa mtandao.
Naye Kamishna wa Ulinzi wa Taarifa za Mtandaoni kutoka Ujerumani, Dkt. Tino Nauman, alisema kuwa anafahamu kuwa Tanzania ina sheria inayolinda taarifa binafsi za watu, sawa na Ujerumani na nchi nyingine nyingi. Aliongeza kuwa uwepo wa sheria kama hiyo ni jambo muhimu sana kwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali.
Alieleza kuwa taarifa yoyote inayomhusu mtu binafsi, kwa mujibu wa sheria, inachukuliwa kuwa taarifa binafsi. Alitoa mifano ya taarifa hizo kuwa ni pamoja na umri wa mtu, namba ya utambulisho, mawasiliano ya mtu na mtu mwingine, barua pepe, na taarifa nyinginezo zinazomhusu mtu moja kwa moja.
Baadhi ya washiriki, akiwemo Bi Sarah Mwaisumo, ambaye ni Mhadhiri Msaidizi katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), walieleza juhudi zinazofanywa katika kuhakikisha wanafunzi wanakuwa wataalamu wabobezi katika masuala ya ulinzi wa mtandao. Alisema kuwa serikali imewekeza katika maabara ya kisasa ya TEHAMA chuoni hapo.
Aliongeza kuwa maabara hiyo inawasaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo masuala mbalimbali ya kidijitali, ikiwemo ulinzi wa taarifa na usalama wa kimtandao, ili waweze kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.