Wakati Tanzania ikijiandaa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Jukwaa la Utawala la Usimamizi wa Kimtandao Barani Afrika (AfIGF) kwa mara ya kwanza, mtaalamu wa masuala ya usalama wa mtandao, Yusuph Kileo, ametoa mbinu muhimu za kujikinga na udukuzi wa mawasiliano ya simu na mitandao mbalimbali.
Kileo ameshauri watumiaji wa simu na mitandao kuimarisha ulinzi kwa kutumia nywila (password) ambazo ni ngumu kubashiriwa na watu wengine. Pia, amewataka watu kuwa waangalifu na kuepuka kubonyeza viungo (links) vinavyotumwa kwenye mitandao bila uhakika wa usalama wake. Zaidi ya hayo, amesisitiza umuhimu wa kuwa na alama maalum za kuingia kwenye akaunti binafsi ambazo zitasaidia kuzuia uingiliaji usioidhinishwa.
Akizungumzia hatua za haraka za kuchukua pale mtu anapogundua kuwa amedukuliwa, Kileo amesema kuwa jambo la kwanza ni kubadilisha nywila mara moja. “Kuhusu kujilinda kwenye mitandao, ni kweli kumekuwa na changamoto ya watu kuhakiwa. Tunashauri kwamba kama ambavyo tunaweka ulinzi kwenye mambo mengine ya kawaida, basi hata kwenye mitandao au mawasiliano yetu tunapaswa kufanya hivyo,” alisisitiza Kileo.
Mtaalamu huyo alitoa elimu hii muhimu jana katika warsha iliyoandaliwa kwa ajili ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Warsha hii ilikuwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Mkutano wa AfIGF, ambao unatarajiwa kufanyika nchini Tanzania kuanzia Mei 29 hadi 31 mwaka huu.
“Huu ni mkutano muhimu sana na nchi yetu imepata bahati kubwa kuwa mwenyeji kwa mara ya kwanza. Hii inaonyesha kuwa Tanzania inafanya vizuri katika eneo hili la usimamizi wa mtandao. Mkutano huu ni kwa ajili ya kila mtu kuja kujadili matumizi sahihi na salama ya mtandao,” alifafanua Kileo.
Aliongeza kuwa miongoni mwa mada zitakazojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na usalama wa mitandao, kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika katika eneo hili, kuboresha miundombinu ya teknolojia, kujadili teknolojia zinazoibukia, na kuhakikisha kuwa kila mtu anapata fursa ya kutumia mtandao.
Kwa upande wake, Bwana Leo Magomba, Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, alisema kuwa mkutano huo utajadili pia masuala yanayohusu Akili Bandia (Artificial Intelligence). “Tutaangalia pia masuala ya Akili Bandia. Tunafahamu kuwa ni teknolojia muhimu sana ambayo inawezesha utendaji kazi, hasa katika kipindi hiki cha mapinduzi ya nne, tano, na sita ya viwanda. Tunahitaji sana teknolojia hii ili kuhakikisha kazi zetu zinafanyika kwa ufanisi, haraka, na kwa umakini katika kufanikisha masuala yote ya kijamii na kiuchumi,” alieleza Magomba.
Alitoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo ili kujifunza kuhusu teknolojia hii mpya, kwani kutakuwa na maonyesho mbalimbali. “Tunaamini kuwa watu wakijifunza vizuri kuhusu Akili Bandia, tutapata wabunifu wengi zaidi nchini,” aliongeza Magomba.
Daktari Nazar Kirama, Mratibu wa Kitaifa wa Jukwaa la Usimamizi wa Intaneti kwa upande wa Tanzania, alisema kuwa zaidi ya watu 1000 kutoka nchi mbalimbali za Afrika na wengine kutoka nchi 10 za Ulaya wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huo. Alisema kuwa vijana kutoka sehemu mbalimbali za Afrika pia watashiriki, na mada nyingine muhimu zitakazojadiliwa ni sera za nchi zinazohusiana na usimamizi wa intaneti. “Huu ni mfumo wa kimataifa ambao unaanzia Umoja wa Mataifa, unakuja Afrika, na kisha unashuka hadi ngazi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alieleza Dk. Kirama.
Mkutano huu unatarajiwa kuwa fursa muhimu kwa wadau mbalimbali kujadiliana kuhusu mustakabali wa usimamizi wa mtandao barani Afrika na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza, ikiwa ni pamoja na masuala ya usalama wa mtandao.