Songwe na Mbeya: Nguzo Mpya za Uchumi Zinavyoifanya Tanzania Kitovu cha Biashara kwa Nchi za SADC

economy | Wed Sep 24 2025


Songwe na Mbeya: Nguzo Mpya za Uchumi Zinavyoifanya Tanzania Kitovu cha Biashara kwa Nchi za SADC

Wakati mataifa mengi barani Afrika yakikabiliwa na changamoto ya gharama kubwa za usafirishaji zinazokwamisha biashara, Tanzania imeibuka kama mfano wa kuigwa, ikijipambanua kama kitovu kikuu cha biashara na usafirishaji kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zisizo na bandari. Kiini cha mapinduzi haya ya kiuchumi ni maboresho makubwa katika Bandari ya Dar es Salaam na uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, hususan Songwe na Mbeya.


Msingi wa mafanikio haya ulianzia katika Bandari ya Dar es Salaam, ambayo imepitia mabadiliko ya kihistoria kati ya mwaka 2021 na 2025. Uwezo wa kuhudumia shehena umepanda kutoka tani milioni 17.05 hadi kufikia tani milioni 27.76. Muhimu zaidi, muda ambao meli zilikua zikisubiri kushusha mizigo umepungua kutoka wastani wa siku 46 hadi siku saba pekee, hatua iliyoifanya bandari hii kuwa kivutio kikuu kwa wafanyabiashara wa nchi jirani kama Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Malawi na Zimbabwe.


Nguvu ya bandari hii inaelekezwa kupitia mishipa mikuu ya kiuchumi iliyopo katika mikoa ya Songwe na Mbeya. Mikoa hii sasa ni nguzo mpya za uchumi wa taifa kutokana na uwepo wa miundombinu muhimu kama mipaka ya Tunduma na Kasumulu, barabara kuu ya TANZAM, reli ya kihistoria ya TAZARA, na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe. Kupitia hapa, Tanzania inahudumia soko lenye zaidi ya watu milioni 168, huku mpaka wa Tunduma ukitajwa kuwa ndio unaohudumia mizigo mingi zaidi Afrika Mashariki.


Ili kuimarisha nafasi hii ya kimkakati, serikali imewekeza mabilioni ya shilingi katika kuboresha miundombinu. Upanuzi wa barabara muhimu kama ya Igawa–Tunduma na ufungaji wa skana za kisasa za X-ray katika mpaka wa Tunduma umepunguza muda wa ukaguzi wa mizigo kwa asilimia 40. Zaidi ya hayo, mfumo wa kidijitali wa kituo cha huduma za pamoja mipakani (OSBP) umefanya mapinduzi kwa kupunguza muda wa kuvuka mpaka kutoka siku nne hadi chini ya siku moja.


Akiweka wazi dira ya siku zijazo, mgombea urais kupitia CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendeleza mafanikio haya kwa miradi mikubwa zaidi. Miongoni mwa ahadi zake ni ujenzi wa Bandari Kavu ya kisasa huko Songwe, ufungaji wa milango ya kisasa ya kielektroniki (smart gates) ili malori yavuke mpaka ndani ya saa 24, na ufufuaji wa kihistoria wa reli ya TAZARA kupitia ubia wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.4 (takriban TZS trilioni 3.6).


Fursa zinazotokana na uwekezaji huu ni nyingi. Tayari biashara kati ya Tanzania na DRC imekua kwa zaidi ya asilimia 180, ambapo bidhaa nyingi kama nafaka na saruji zinatoka Mbeya na Songwe. Kukamilika kwa miradi hii kutapunguza gharama za usafiri kwa zaidi ya asilimia 68, kutafungua masoko kwa wakulima, na kuongeza ajira. Hata hivyo, bado kuna kazi ya kufanya, ikiwemo kujenga maegesho ya malori, kuhakikisha huduma za kibenki zinapatikana saa 24 mipakani, na kupunguza idadi ya mizani barabarani ili kurahisisha zaidi mtiririko wa biashara.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.