Mlipuko wa matumizi ya simu janja na intaneti, ukuaji wa kasi wa sekta ya wajasiriamali wadogo na wa kati, pamoja na msukumo wa kitaifa wa ujumuishaji wa kifedha, vimetajwa kuwa nguzo tatu kuu zilizoibeba Tanzania na kuifanya kuwa nchi yenye mazingira bora ya ukuaji wa malipo ya kidijitali barani Afrika.
Uchambuzi huu umetolewa na kampuni kubwa ya malipo ya kidijitali duniani, Visa, ambayo imetangaza rasmi ufunguzi wa ofisi zake nchini Tanzania. Hatua hii imetajwa kuwa ishara ya imani kubwa waliyonayo katika mustakabali wa uchumi wa kidijitali wa nchi.
Akizungumza Dar es Salaam leo, Julai 16, 2025, katika maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Visa Tanzania, Mkuu wa Visa kwa Ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika, Michael Berner, alisema mambo hayo matatu yameifanya Tanzania kuwa soko la kimkakati na la kuvutia kwao.
"Tunaona fursa kubwa hapa. Ongezeko la matumizi ya simu, nguvu ya wajasiriamali, na sera za serikali za ujumuishi wa kifedha vinatengeneza mfumo wa malipo wenye ubunifu na unaowafikia watu wote. Kufungua ofisi hapa kutatuwezesha kushirikiana kwa karibu zaidi na mabenki, fintech, na serikali ili kukuza matumizi ya malipo ya kisasa," alisema Berner.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Emmanuel Tutuba, ambaye alisisitiza kuwa serikali imejipanga kikamilifu katika safari hii ya kidijitali. Alisema serikali, kupitia Mpango wa Miaka 10 wa Ujumuishaji wa Kifedha, imeweka miongozo thabiti inayosimamia malipo ya kidijitali ili kuhakikisha huduma zinakuwa salama na zinawafikia wananchi wengi zaidi.
"Lengo letu ni kuhakikisha Tanzania inafikia uchumi wa kidijitali kikamilifu. Hii itarahisisha huduma za kifedha, kukuza biashara, na kusaidia ukuaji wa uchumi wa taifa letu," alisema Profesa Tutuba.
Maadhimisho hayo ya Siku ya Visa, yaliyokuwa na kaulimbiu "Kujenga Mustakabali wa Malipo Nchini Tanzania," yamewakutanisha wadau muhimu kutoka sekta ya fedha na teknolojia, kuashiria mwanzo mpya wa ushirikiano utakaoharakisha safari ya Tanzania kuelekea kuachana na matumizi ya fedha taslimu.