Waziri wa Fedha wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa agizo kali kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhakikisha kuwa benki zote na taasisi za fedha nchini zinajiunga na Mfumo mpya wa Kushughulikia Malalamiko ya Watumiaji wa Huduma za Fedha. Waziri alisisitiza kuwa mfumo huu utakuwa chachu muhimu katika kutatua kero za wateja na kuimarisha uwazi katika utoaji wa huduma za kifedha.
Dkt. Nchemba alitoa maagizo haya muhimu wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa 'Sema na BoT' na Mazingira ya Majaribio ya Teknolojia ya Fedha (Bank of Tanzania Fintech Regulatory Sandbox), hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage jijini Dodoma. Akizungumzia kwa undani mfumo wa 'Sema na BoT', Waziri alieleza kuwa utatoa jukwaa maalum la kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha kwa ufanisi, uwazi, na kwa wakati. Mfumo huu unatarajiwa kuwa suluhisho la kero mbalimbali, ikiwemo malalamiko yanayohusu mikopo yenye masharti magumu au "kausha damu."
Aliongeza kuwa mfumo wa 'Sema na BoT' utaimarisha imani ya wananchi katika kutumia huduma rasmi za kifedha na kuongeza uwajibikaji kutoka kwa watoa huduma za fedha wanaosimamiwa na BoT. Pamoja na hayo, Dkt. Mwigulu aliwataka watoa huduma za fedha kuhakikisha wanatoa elimu sahihi ya fedha kwa wateja wao na umma kwa ujumla, kama inavyoelekezwa na Kanuni za Benki Kuu za Kumlinda Mtumiaji wa Huduma za Fedha za mwaka 2019.
Kuhusu kuanzishwa kwa Mazingira ya Majaribio ya Teknolojia ya Fedha (Fintech Regulatory Sandbox), Dkt. Nchemba alifafanua kuwa Serikali imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa kinara wa ubunifu wa teknolojia ya kifedha miongoni mwa nchi zinazoendelea. Lengo ni kuweka mazingira yanayovutia uwekezaji wa kiteknolojia na kuwajengea uwezo vijana wa Kitanzania kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa kidijitali. "Kuanzishwa kwa Mazingira ya Majaribio ya Teknolojia ya Fedha kunadhihirisha dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye anatamani kukuza matumizi ya teknolojia katika sekta ya fedha kuelekea kwenye uchumi wa kidijitali," alisema Dkt. Nchemba, akisisitiza dira ya Rais Samia.
Aidha, aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupokea elimu ya fedha inayotolewa na taasisi za fedha. Alisema elimu hiyo itawasaidia kuwa na uelewa mpana wa masuala ya kifedha na kuepuka kujihusisha na huduma zenye masharti yasiyo rafiki.
Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, alitoa ahadi kuwa watasimamia kikamilifu mfumo huo mpya ili kuhakikisha unatoa matokeo yaliyokusudiwa. Naye Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, alielezea mfumo wa 'Sema na BoT' kama mfumo rafiki, utakaomwezesha kila mtumiaji wa huduma za fedha kuufikia na kuutumia wakati wowote, bila kujali mahali alipo au uelewa wake wa teknolojia. Aliongeza kuwa mfumo huo utazisaidia taasisi za fedha kubaini na kushughulikia malalamiko ya wateja wao kwa wakati, hatua itakayoboresha utoaji wa huduma kwa ujumla.