Wakati mjadala wa faida na hasara za ubinafsishaji wa mashirika ya umma ukiendelea kuwa somo muhimu barani Afrika, Kampuni ya TPC ya Moshi mkoani Kilimanjaro imesimama kidete kama kielelezo cha mafanikio makubwa ya Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) nchini Tanzania.
Hayo yamebainishwa wazi wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 25 ya ubia huo wenye historia ya kipekee, ambapo Msajili wa Hazina, Bwana Nehemia Mchechu, amefichua kuwa uamuzi wa serikali wa mwaka 2000 wa kuuza asilimia 75 ya hisa zake kwa wawekezaji binafsi, sasa unalipa mabilioni. Katika gawio la mwaka huu pekee, serikali imetabasamu baada ya kukabidhiwa hundi ya Shilingi bilioni 16.5.
Kutoka Tani 36,000 hadi Rekodi ya Dunia
Akichambua safari ya robo karne ya uwekezaji huo, Bwana Mchechu amebainisha kuwa kabla ya ubia, uzalishaji ulikuwa ukisua sua. Mwaka 2000, kiwanda hicho kilikuwa kikitengeneza tani 36,000 tu za sukari kwa mwaka. Leo hii, kupitia uwekezaji wa kisasa na usimamizi makini, uzalishaji umepaa hadi kufikia tani 120,000 kwa sasa.
Hata hivyo, sifa kubwa ya TPC haiko kwenye wingi tu, bali kwenye ufanisi. Mchechu amebainisha kuwa kampuni hiyo imewekeza kiasi cha zaidi ya Shilingi bilioni 265 kuboresha miundombinu ya mashamba na teknolojia.
"Uwekezaji huu umewezesha TPC kufikia uzalishaji wa wastani wa tani 150 za miwa kwa hekta moja. Huu ni ufanisi wa hali ya juu sana unaotambuliwa kama miongoni mwa viwango bora kabisa Afrika na duniani. Hii inathibitisha kuwa tukiweka mazingira sawa, Tanzania inaweza kuwa kinara wa kilimo biashara duniani," alisisitiza Mchechu.
Mchango kwa 'Keki ya Taifa' na Ajira
Mbali na gawio la moja kwa moja, Msajili wa Hazina ameeleza kuwa faida za kiuchumi za TPC ni pana zaidi. Mwaka 2023 pekee, mbali na gawio la Bilioni 16.5, kampuni hiyo ilichangia zaidi ya Shilingi bilioni 75 kwenye kapu la serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali.
Kwa upande wa ajira, TPC imegeuka kuwa mwajiri mkubwa kaskazini mwa Tanzania, ikitoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa Watanzania zaidi ya 4,000. Hii inaenda sambamba na miradi ya kurudisha fadhila kwa jamii (CSR) katika sekta za elimu, afya, na miundombinu, jambo linaloimarisha ustawi wa wananchi wa Moshi na maeneo jirani.
Kiwanda Kipya cha Bilioni 130 na Mwekezaji Mpya
Sherehe hizo hazikuishia kwenye hotuba na keki tu. Bwana Mchechu alishuhudia uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya mradi mpya na wa kimkakati wa 'TPC Distillery'. Mradi huu unaolenga kuchakata 'molasesi' (masalia ya miwa) unagharimu Dola za Marekani milioni 52 (sawa na takribani Shilingi bilioni 130).
Katika mradi huu mpya, muundo wa umiliki umebadilika kidogo ili kuleta ujuzi mpya. Serikali na TPC zitamiliki asilimia 85 ya hisa, huku mwekezaji mpya, kampuni ya Isautier Drinks Africa, ikichukua asilimia 15. Hii ni ishara ya wazi ya imani ya wawekezaji wa kimataifa katika uthabiti wa sera za uchumi za Tanzania chini ya uongozi wa sasa.
Sauti za Wawekezaji na Serikali ya Mkoa
Mwenyekiti wa Miwa Group, Bwana Arnaud Lagesse, amesema mafanikio haya si kwamba hayakuwa na changamoto. Kampuni imepitia vipindi vigumu vya ukame na misukosuko ya soko la dunia, lakini ustahimilivu na maono ya pamoja ndiyo yameifikisha hapo ilipo.
"Ujenzi wa kiwanda hiki kipya cha kuchakata molasesi ni sehemu ya mkakati wetu mpana wa kuongeza thamani (value addition). Hatutaki kuishia kwenye sukari tu, tunataka kutumia kila kinachotokana na muwa kuzalisha nishati na bidhaa nyingine," alisema Lagesse.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro (RAS), Bwana Kiseo Nzowa, amepongeza hatua hiyo akisema ni ushindi kwa mkoa. "Mradi huu mpya utaongeza ajira, utakuza mapato ya kodi, na muhimu zaidi, utaifanya Tanzania kuwa mshindani mkubwa katika soko la kikanda la bidhaa za sukari na nishati," alihitimisha Bwana Nzowa.
Miaka 25 ya TPC ni funzo kuwa, ubinafsishaji ukisimamiwa vizuri, unaweza kuwa na tija kubwa kwa taifa, wawekezaji, na wananchi kwa ujumla.