Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Ashatu Kijaji, amezindua rasmi mnada wa Mpakani Kileo, uliopo wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro, mnada ambao unatarajiwa kuwa chachu ya kuongeza masoko ya mifugo kwa wafugaji na wafanyabiashara wa eneo hilo. Mnada huu, ambao una uwezo wa kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi, una miundombinu muhimu kama vile uzio wa mzunguko wa mita 500, kipakilio, mazizi, choo, na miundombinu ya maji, na umegharimu shilingi milioni 208.924 hadi kukamilika.
"Mnada huu una uwezo wa kupokea ng'ombe 500 na mbuzi na kondoo 3000 kwa wakati mmoja. Nina imani kuwa uwekezaji huu utaleta tija kubwa, na miundombinu iliyojengwa itatunzwa na kulindwa," alisema Dk. Kijaji wakati wa uzinduzi. Aliongeza kuwa ujenzi wa mnada huo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira njema ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa wafugaji na wadau wa mifugo nchini, kwa lengo la kupanua masoko ya mifugo ndani na nje ya nchi.
Dk. Kijaji alifahamisha kuwa hadi sasa, minada ya mifugo 51 yenye thamani ya shilingi bilioni 17.5 imejengwa na kukarabatiwa nchini, hatua ambayo imewezesha ongezeko kubwa la biashara ya mifugo. Kutokana na uwepo wa minada hiyo, mifugo iliyouzwa imeongezeka kutoka thamani ya shilingi trilioni 1.5 mwaka 2021/22 hadi kufikia shilingi trilioni 3.7 mwaka 2024/25.
Aidha, Waziri huyo aliwataka wafanyabiashara wa mifugo, hasa wale wanaosafirisha mifugo nje ya nchi, kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu za nchi katika kufanya biashara hiyo. Alionya kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao hufanya biashara kinyume na taratibu na kutumiwa na wafanyabiashara kutoka nchi jirani kununua na kutorosha mifugo kwa siri kupitia njia zisizo rasmi.
"Wakati mwingine, wafanyabiashara kutoka nchi jirani huingia na kwenda moja kwa moja kwenye minada ya awali kwa kuwatumia wenyeji kununua mifugo na kuisafirisha kinyume na taratibu. Hii ni kosa kisheria," alisisitiza Dk. Kijaji. Aliongeza kuwa wale wanaofanya hivyo wanahujumu mapato ya serikali na kudidimiza ustawi wa sekta ya mifugo nchini, na serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi yao.
Dk. Kijaji pia aliwataka watendaji wa serikali wanaosimamia minada na vituo vya ukaguzi wa mifugo kutoa vibali vya biashara kwa mujibu wa sheria ili kuepusha usumbufu kwa wafanyabiashara.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Abdul Mhinte, alisema mnada wa Mpakani Kileo ni moja ya minada 10 ya kimkakati iliyopo mipakani mwa nchi, ikiwa ni pamoja na minada iliyopo Songea, Kagera, Tanga, Arusha, na maeneo mengine.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, aliahidi kuwa mkoa huo utashirikiana na halmashauri zote kuhakikisha miundombinu ya mnada inalindwa na kutunzwa.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mwanahamisi Munkunda, alimshukuru Rais Dk. Samia na Waziri Dk. Kijaji kwa kujenga na kuboresha mnada huo, ambao utaongeza pato kwa wafugaji, wafanyabiashara, na nchi kwa ujumla.