Mapinduzi ya Usafiri Baharini: Safari ya Dar-Zanzibar Kuwa Dakika 45, Watu Kufanya Kazi Miji Miwili

economy | Thu Aug 28 2025


Mapinduzi ya Usafiri Baharini: Safari ya Dar-Zanzibar Kuwa Dakika 45, Watu Kufanya Kazi Miji Miwili

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza mradi kabambe wa ujenzi wa bandari mpya ya abiria katika eneo la Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, mradi unaotarajiwa kupindua kabisa taswira ya usafiri kati ya Dar es Salaam na Visiwani. Kukamilika kwa mradi huu ifikapo mwaka 2027 kutapunguza muda wa safari kutoka saa mbili za sasa hadi dakika 45 pekee.


Akifafanua kuhusu mradi huo, Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar, Akif Ali Khamis, alisema bandari hiyo itafungua njia mpya ya usafiri, ambapo boti za mwendo kasi zitaanzia Kizimkazi na kutia nanga katika eneo la Kunduchi Ununio jijini Dar es Salaam, badala ya njia ya sasa ya kutoka Bandari ya Malindi hadi Kivukoni.


Athari za mradi huu zinatajwa kuwa kubwa kiuchumi na kijamii. Bwana Khamis alieleza kuwa urahisi na kasi ya usafiri utawawezesha wananchi kuishi upande mmoja wa Muungano na kufanya kazi upande wa pili, wakisafiri kila siku. "Mtu ataweza kuishi Zanzibar na anakuja kufanya kazi Dar es Salaam na kurudi jioni, au kinyume chake. Hii itafungua fursa nyingi za kiuchumi na kuimarisha zaidi uhusiano wetu kama taifa moja," alisema. Aliongeza kuwa hatua hii ni utekelezaji wa vitendo wa azma ya kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa zaidi ya miaka 60 iliyopita.


Wakati mradi wa Kizimkazi ukisubiriwa kwa hamu, Serikali ya Zanzibar pia imetenga kiasi cha Dola za Marekani milioni 250 (takriban Shilingi za Tanzania Bilioni 650) kwa ajili ya ujenzi wa bandari nyingine mpya na ya kisasa ya abiria katika eneo la Maruhubi, Mjini Unguja. Bandari hii inatarajiwa kuanza kutoa huduma ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2025, ikiwa ni mkakati wa haraka wa kupunguza msongamano mkubwa unaoikabili Bandari ya Malindi kwa sasa.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.