Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewasha rasmi mtambo mpya unaozalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa megawati 20 katika kituo cha Mtwara II. Hatua hii inatajwa kuleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma ya nishati katika ukanda wa Kusini mwa Tanzania.
Uzinduzi huu ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa serikali wa kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu na endelevu kote nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Uzalishaji TANESCO, Mhandisi Antony Mbushi, alieleza kuwa mradi huo ni sehemu ya mpango wa shirika wa kuimarisha miundombinu ya uzalishaji.
"Awali kituo cha Mtwara kilikuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 50. Sasa tumeongeza megawati 20, hivyo kufikia megawati 77.5," alisema Mhandisi Mbushi, akifafanua kuwa uwezo huo sasa unazidi mahitaji ya juu ya sasa ya mkoa huo ambayo ni megawati 38.5 pekee. Uwezo huo mkubwa utatosheleza mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Fursa Mpya za Uwekezaji Zafunguka
Uzinduzi wa mtambo huu wa gesi asilia unatarajiwa kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika mikoa ya Mtwara na Lindi, huku ukitoa matumaini mapya kwa wananchi kupitia upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa shughuli za uzalishaji, biashara, na uwekezaji.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Sawala, aliishukuru serikali, akimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa miradi ya nishati inayowanufaisha wananchi wa Kusini.
"Tuna kila sababu ya kumpongeza na kumshukuru Rais wetu... Hii ni hatua muhimu katika kuinua maisha ya wananchi wetu na kuchochea maendeleo ya viwanda katika mikoa ya Lindi na Mtwara," alisema Kanali Sawala.
Alisisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kunatoa fursa kubwa kwa wawekezaji kutumia rasilimali ya umeme wa uhakika kujenga viwanda na kuendeleza shughuli za kiuchumi. "Sasa tuna umeme wa kutosha, ni wakati muafaka kwa wawekezaji kuja kujenga viwanda," alihimiza Kanali Sawala.