Safari ya Tanzania kuelekea kuongeza uzalishaji wa gesi asilia imepiga hatua muhimu nchini China, baada ya wataalamu kutoka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kukamilisha ukaguzi na majaribio ya mtambo mpya na wa kisasa utakaotumika kuchimba visima vitatu katika Kitalu cha Mnazi Bay, mkoani Mtwara.
Ukaguzi huo wa kina, uliofanyika katika jimbo la viwanda la Tianjin nchini China, ni hatua ya kimkakati ya PURA kuhakikisha vifaa vyote vinavyoletwa nchini kwa ajili ya shughuli za utafutaji na uchimbaji vinakidhi viwango vya juu vya ubora na usalama kabla ya kuanza kazi.
Mtambo huo, wenye uwezo wa kuchimba hadi kina cha mita 8,000 chini ya ardhi, ulifanyiwa majaribio mbalimbali mbele ya wataalamu wa PURA, ambao waliridhishwa na ufanisi wake. Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, kufanya ukaguzi katika nchi unapoundwa mtambo huo kunatoa hakikisho na kuepusha uwezekano wa kuletwa kwa mitambo isiyo na ubora, jambo ambalo linaweza kuchelewesha miradi na kuleta hasara kwa taifa.
PURA, kama msimamizi mkuu wa shughuli za utafutaji na uchimbaji wa petroli na gesi nchini, imesisitiza kuwa inafuatilia kila hatua ya mradi huu muhimu ili kuhakikisha unatekelezwa kama ilivyopangwa na kwa viwango vya kimataifa.
Kazi ya uchimbaji wa visima hivyo vitatu inatarajiwa kuanza rasmi Novemba 2025. Kukamilika kwa mradi huu kunatarajiwa kuongeza uzalishaji wa gesi asilia nchini kwa zaidi ya futi za ujazo milioni 30 kwa siku, hatua itakayochochea upatikanaji wa nishati na kusaidia ukuaji wa viwanda na uchumi wa Tanzania.