Kutoka Mitumbwi Hadi Madaraja: Neema ya TARURA Yabadili Maisha Bagamoyo

economy | Thu Nov 13 2025


Kutoka Mitumbwi Hadi Madaraja: Neema ya TARURA Yabadili Maisha Bagamoyo

Kwa miaka mingi, wakazi wa baadhi ya maeneo katika Wilaya ya Bagamoyo, msimu wa mvua ulikuwa ukileta kero kubwa na hata hatari kwa maisha. Hali hii inathibitishwa na Bi. Cristina Kasimangi, mkazi wa Mkunguni, ambaye anakumbuka kwa uchungu jinsi walivyolazimika kutumia usafiri duni na wa hatari kuvuka mito.


"Zamani tulikuwa tunavuka kwa mitumbwi, ilikuwa hatari sana," anakiri Bi. Kasimangi. Hali hii ilimaanisha kuwa shughuli za msingi za kijamii zilikuwa za kubahatisha; watoto walishindwa kwenda shule na wagonjwa walikabiliwa na changamoto kubwa kufika vituo vya afya.


Hata hivyo, kilio chao sasa kimesikika. Bi. Kasimangi anaeleza kwa furaha kwamba hali imebadilika kabisa. "Sasa watoto wanaenda shule bila shida na wagonjwa wanafika hospitali kwa urahisi," anasema.


Mabadiliko haya makubwa ni matokeo ya uwekezaji mkakati uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Wananchi wa Bagamoyo wametoa shukrani za dhati kwa serikali kwa kuelekeza fedha za maendeleo kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), ambazo zimefungua milango ya fursa kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara na madaraja.


Akifafanua kuhusu mafanikio hayo, Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Bagamoyo, Mhandisi Bernard Mwita, amesema miradi hii imekuwa mkombozi halisi kwa wananchi. Amesema uwekezaji huo umeboresha kwa kiwango kikubwa huduma za usafiri na kufungua fursa nyingi za kiuchumi, hasa kwa wananchi waishio vijijini.


"Miradi hii imekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wetu. Sasa wanapata huduma za kijamii kwa urahisi kipindi chote cha mwaka, tofauti na awali ambapo maeneo mengi yalikuwa hayapitiki hasa wakati wa mvua,” alisisitiza Mhandisi Mwita.


Miongoni mwa miradi mikubwa iliyokamilika na kuleta ahueni ni pamoja na daraja la miguu mitatu lenye urefu wa mita 16.4, lililopo katika barabara ya Milo. Ujenzi wa daraja hili, uliofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya shilingi milioni 499.8, umekamilika kwa asilimia mia moja na tayari limeanza kutumika.


Aidha, Mhandisi Mwita alitaja kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa barabara muhimu ya Ruvu–Milo yenye urefu wa kilometa 11. Mradi huu, uliogharimu shilingi milioni 253.6, ulihusisha ujenzi wa madaraja makubwa mawili na makalvati manne. Kukamilika kwake kumeondoa kabisa changamoto ya usafiri, na sasa barabara hiyo inapitika mwaka mzima bila kujali hali ya hewa.


Uwekezaji huu umegusa pia sekta ya kilimo moja kwa moja. Msimamizi wa miradi kutoka TARURA Bagamoyo, Mhandisi Philimo David, alieleza kuhusu mradi wa barabara ya Makofia–Kimalang’ombe. Mradi huu wa kilometa 2 zilizojengwa kwa kiwango cha changarawe, pamoja na daraja moja, umekamilika kikamilifu. Utekelezaji wake ulifanywa na mkandarasi Lutavi Construction Company Ltd kwa gharama ya shilingi milioni 121.9.


"Mradi huu umesaidia sana kupunguza changamoto za usafirishaji wa mazao na kuwafungulia wananchi fursa za kiuchumi. Wakulima sasa wanauza mazao yao kwa urahisi na kufika masokoni bila vikwazo,” alieleza Mhandisi Philimo.


Wakati wananchi wakifurahia matunda haya, Mhandisi Mwita ametoa wito kwao, akiwaomba kutunza miundombinu hiyo. "Tunawaomba wananchi waendelee kutunza miundombinu hii, kwa kuwa ni mali yao na ni muhimu kwa maendeleo ya jamii,” aliongeza. TARURA Bagamoyo imeahidi kuendelea kusimamia miradi yote kwa karibu ili kuhakikisha wananchi wanapata thamani halisi ya fedha za kodi zao.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.