Kwa miaka mingi, maeneo ya Goba, Msumi, na Tegeta A jijini Dar es Salaam yamekuwa yakikabiliwa na kitendawili kigumu; eneo linalokua kwa kasi na kujengwa majumba ya kifahari, lakini miundombinu yake ya barabara ikiwa ni "kero sugu" inayowatesa wakazi wake, hasa nyakati za mvua. Hata hivyo, upepo wa mabadiliko umeanza kuvuma kwa kasi ya ajabu, ukileta tabasamu jipya kwa wananchi wa maeneo hayo.
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), chini ya usimamizi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita, wameingia "chimbo" na kuanza mageuzi makubwa ya miundombinu ambayo yanatajwa kuwa mkombozi wa uchumi wa wakazi wa Goba na vitongoji vyake. Mradi huu wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami unahusisha njia muhimu za Wakorea–Goba, Msumi, na Goba–Mkorea, ambazo kwa muda mrefu zamekuwa kero kwa watumiaji wa vyombo vya moto na watembea kwa miguu.
Akizungumzia maendeleo ya miradi hiyo ambayo imezua gumzo la furaha mitaani, Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Geofrey Mkinga, ameweka wazi kuwa kazi inakwenda kwa kasi ya "kufa mtu". Mkinga amebainisha kuwa ujenzi wa barabara ya Wakorea–Goba yenye urefu wa kilomita 9.9 umefikia hatua ya kuridhisha na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Agosti mwaka huu.
"Tulianza kazi hii mwezi wa tano na tunatarajia kukabidhi mradi mwezi wa nane. Hii ni spidi kali yenye lengo la kutoa ahueni ya haraka kwa wakazi wa maeneo haya ambao wameteseka kwa muda mrefu," alisisitiza Mhandisi Mkinga.
Mbali na lami hiyo, habari njema zaidi inakuja kwa wakazi wa Tegeta A Mpakani, ambapo ujenzi wa daraja la kisasa unaendelea. Daraja hili limekuwa "mwiba" kwa wananchi, likijaa maji na kukata mawasiliano kila anga linapochafuka (mvua zinaponyesha). Kukamilika kwake kutafungua mawasiliano ya kudumu na kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi bila kujali majira ya mwaka.
Katika muktadha mpana, TARURA imebainisha kuwa miradi hii ni sehemu ya mpango mkakati wa kuboresha jumla ya kilomita 750 za barabara ndani ya jiji la Dar es Salaam, huku usanifu wa kilomita 259 ukiwa tayari umekamilika. Kwa upande wa Manispaa ya Ubungo, barabara ya Goba–Mkorea inayojengwa na kampuni ya Zhongmei Group nayo inarindima, huku Mhandisi wa mradi, Amani Alex, akihakikisha viwango vya kimataifa vinazingatiwa.
Wakazi wa eneo hilo hawajaficha hisia zao. Bi. Janeth Mgaya, mkazi wa Goba Mpakani, ameeleza kuwa kukamilika kwa barabara hizi kutakuwa mkombozi wa mifuko yao.
"Huku usafiri ni shida, kuna daladala moja tu inayotuhudumia. Hali hii inatufanya tutegemee bajaji ambazo zinatutoza zaidi ya Shilingi 2,000 kwa safari fupi. Hii ni gharama kubwa kwa mwananchi wa kawaida. Tunashukuru sana serikali, lami hii itashusha gharama na kuleta daladala nyingi," alisema Bi. Janeth kwa matumaini.
Wachumi wanasema kuwa kufunguka kwa barabara hizi hakutapunguza tu msongamano na gharama za usafiri, bali pia kutapandisha thamani ya ardhi na nyumba katika maeneo ya Goba na Msumi, na kuvutia wawekezaji zaidi wa biashara ndogo na za kati. Hii ni tafsiri halisi ya dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya "Kazi Iendelee" kwa vitendo, ikilenga kuboresha maisha ya kila Mtanzania kupitia miundombinu bora.