Hofu na hasira zimetanda miongoni mwa wakazi wa Mtaa wa Tegeta "A," katika Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam, kufuatia ongezeko la ghafla la nauli ya usafiri wa Daladala na Bajaji za kuchangia. Nauli imepanda kutoka TZS 500 hadi TZS 1,000, ongezeko ambalo wananchi wanasema limewaathiri vibaya, hasa wafanyakazi wenye kipato duni na wanafunzi wanaotegemea usafiri huo kwa shughuli zao za kila siku.
Wakizungumza kwa uchungu, wakazi hao wameeleza kuwa kupanda kwa nauli ni pigo kubwa kwao, kwani kunawaongezea mzigo wa kifedha tayari katika kipindi hiki ambapo hali ya uchumi kwa ujumla ni ngumu. Wamesisitiza kuwa usafiri huo ni muhimu sana kwao katika maisha yao ya kila siku, kwani wengi hutegemea kusafiri kwenda kazini, sokoni, na watoto shuleni. Ongezeko hili la nauli linawagusa moja kwa moja na kupunguza uwezo wao wa kumudu gharama nyingine muhimu za maisha.
Akijaribu kutoa ufafanuzi kuhusu chanzo cha ongezeko hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Tegeta "A," Bwana Protus Ruwanda, amesema kuwa sababu kuu inayosababisha kupanda kwa nauli ni hali mbaya ya miundombinu, hususan barabara. Ubovu wa barabara unawalazimu watoa huduma za usafiri kuingia gharama kubwa za uendeshaji na matengenezo ya vyombo vyao vya usafiri, na hivyo kuamua kupandisha nauli ili kukabiliana na hali hiyo.
"Tunaendelea kufanya mawasiliano na mamlaka zinazohusika ili kuona ni namna gani tunaweza kuboresha barabara hii. Tunafahamu umuhimu wa barabara nzuri kwa wananchi wetu. Hata kama kwa sasa hatuwezi kupata lami, basi angalau barabara ifanyiwe ukarabati wa muda ili kupunguza athari kwa wananchi, hasa katika kipindi hiki cha mvua ambacho kinazidisha ubovu wa barabara," alisema Bwana Ruwanda.
Kwa muda mrefu, wakazi wa Tegeta "A" wamekuwa wakijitahidi kuchangia fedha zao wenyewe kwa ajili ya kufanya ukarabati mdogo wa barabara zao, huku wakiendelea kusubiri utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na serikali za kuweka lami, lakini hadi sasa hakuna mafanikio yoyote yaliyopatikana. Sasa, wanasisitiza kuwa serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti na za haraka kumaliza tatizo hili la miundombinu. Wanasema kuwa kupanda kwa nauli ni mzigo mkubwa ambao unawazuia kujikwamua kiuchumi na kuendeleza maisha yao.
Wananchi hao wameapa kuendelea kushinikiza mamlaka husika kuhakikisha kuwa barabara zao zinaboreshwa kwa kiwango kinachostahili, ili kupunguza gharama za usafiri ambazo kwa sasa zinawanyima raha na kuwafanya maisha kuwa magumu. Wanataka kuona hatua za kweli zikichukuliwa ili kurahisisha maisha yao ya kila siku na kuwezesha shughuli zao za kiuchumi kufanyika kwa urahisi zaidi.