Kampuni nguli ya kibiashara yenye asili ya Tanzania, Amsons Group, imezidi kutanua mbawa zake barani Afrika baada ya kuingia makubaliano ya kihistoria na Serikali ya Zambia yenye lengo la kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika sekta ya nishati. Hatua hii inatajwa kuwa ni ushindi wa kidiplomasia wa kiuchumi kwa Tanzania, huku ikidhihirisha uwezo wa kampuni za wazawa kushindana katika masoko ya kimataifa.
Katika mradi huo ulioteka vichwa vya habari Kusini mwa Afrika, Amsons Group imeingia ubia wa kimkakati na kampuni ya 'Exergy Africa Limited' ya nchini Zambia. Mpango huo kabambe unalenga kuzalisha jumla ya Megawati 1,300 za umeme, hatua inayotazamiwa kuwa mwarobaini wa kudumu wa tatizo la nishati linaloikabili nchi hiyo jirani.
Uwekezaji huo una thamani ya Dola za Marekani milioni 900 (sawa na takribani Shilingi za Kitanzania Trilioni 2.4). Mchanganuo wa fedha hizo unaonesha kuwa Dola milioni 600 (takribani Tsh Trilioni 1.6) zitaelekezwa kwenye ujenzi wa mitambo ya umeme wa jua (Solar) itakayozalisha Megawati 1,000. Aidha, kiasi cha Dola milioni 300 (takribani Tsh Bilioni 800) zimetengwa kwa ajili ya kuzalisha Megawati 300 kutokana na makaa ya mawe.
Hafla yautiliaji saini makubaliano hayo ilifanyika hivi karibuni katika Ikulu ya Zambia jijini Lusaka, ikishuhudiwa na Rais wa nchi hiyo, Hakainde Hichilema, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Amsons Group, Bw. Edha Nahdi. Tukio hili linaashiria imani kubwa ambayo nchi za SADC zinayo kwa wawekezaji kutoka Tanzania.
Akizungumza kwa hisia wakati wa hafla hiyo, Rais Hichilema aliimwagia sifa kemkem kampuni ya Amsons, akibainisha kuwa uwekezaji huo umekuja muda muafaka ambapo Zambia inapambana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi ziliathiri uzalishaji wa umeme wa maji.
"Uwekezaji huu wa Gigawati moja ni mapinduzi ya kweli. Unakuja kukata mzizi wa fitina wa uhaba wa nishati nchini mwetu kwa kutupa umeme wa uhakika na safi usiotegemea huruma ya mvua au kina cha mabwawa ya maji," alisisitiza Rais Hichilema huku akibainisha kuwa mradi huu utahakikisha gridi ya taifa inaimarika na kuchochea ukuaji wa viwanda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Amsons Group, Edha Nahdi, alisema hatua hiyo ni sehemu ya maono mapana ya kampuni hiyo kuhakikisha inavuka mipaka na kupeleka ufanisi wa Kitanzania barani Afrika. Nahdi alieleza kuwa mradi huu si tu biashara, bali ni daraja la undugu na maendeleo.
"Tuko hapa kujenga zaidi ya vituo vya umeme; tunajenga ajira endelevu kwa vijana wa Zambia na Afrika, tunaongeza uwezo wa wataalamu wa ndani, na kuweka mifumo imara itakayohudumia vizazi vijavyo kuanzia mashuleni hadi viwandani," alieleza Nahdi.
Uwekezaji huu unakuja wakati ambapo Amsons Group imejiimarisha kama konglomerati inayoheshimika Afrika Mashariki na Kati, ikijihusisha na sekta mbalimbali zikiwemo usafirishaji, saruji, na ngano. Kuingia kwao kwa kishindo kwenye sifa ya nishati Zambia, nchi ambayo imekuwa ikiteseka na mgawo wa umeme kutokana na ukame kupunguza kina cha maji katika Bwawa la Kariba, ni kielelezo tosha cha ukomavu wa sekta binafsi ya Tanzania.
Mkurugenzi wa Exergy Africa Limited, Monica Musonda, na Waziri wa Nishati wa Zambia, Makozo Chikote, kwa pamoja walipongeza ushirikiano huo wakisema ni kielelezo cha jinsi Waafrika wanavyoweza kutatua changamoto zao wenyewe kwa kushirikiana kibiashara na kuondoa utegemezi wa nje.