Edha Nahdi, mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Amson Group, amefanya mazungumzo muhimu na Rais wa Kenya, William Ruto, katika Ikulu ya Nairobi. Mazungumzo hayo, yaliyofanyika Aprili 18, 2025, yalilenga upanuzi mkubwa wa Kiwanda cha Saruji cha Bamburi Cement, awamu ya pili, uwekezaji ambao unakadiriwa kufikia Dola za Marekani milioni 380, sawa na takribani shilingi bilioni 960 za Kitanzania.
Bi. Edha Nahdi, mwanamke mwenye umri wa miaka 37, ameweka historia kwa kufanikisha ununuzi wa Kampuni ya Bamburi Cement kwa thamani ya shilingi bilioni 500 za Kitanzania, sawa na Dola za Marekani milioni 182. Hatua hii imetambuliwa kama uwekezaji mkubwa zaidi kuwahi kufanywa na Mtanzania nje ya nchi.
Kulingana na vyanzo vya uwekezaji, uwekezaji huu mkubwa unazidi hata ule wa mfanyabiashara maarufu Rostam Aziz, ambaye aliwekeza nchini Kenya kupitia Kampuni ya Taifa Gas kwa Dola za Marekani milioni 130, sawa na takribani shilingi bilioni 338 za Kitanzania. Mkataba wa ununuzi wa Bamburi Cement unatajwa kuwa ni uwekezaji mkubwa zaidi wa kibinafsi kutoka kampuni ya Kitanzania nchini Kenya tangu kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.
Uwekezaji huu unaiwezesha Amson Group kupanua shughuli zake katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki, na kuimarisha nafasi yake kama mzalishaji mkuu wa saruji. Kwa upande mwingine, Amson Group imeonesha nia ya kupanua uwekezaji wake nchini Uganda, baada ya Bamburi Cement kukamilisha uuzaji wa hisa zake kwa asilimia 70 katika kampuni tanzu ya Hima Cement kwa kampuni za Sarrai Group na Rwimi Holding, kwa thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 84, sawa na shilingi bilioni 214 za Kitanzania, mnamo Machi 2024.
Amson Group, inayomilikiwa na familia ya Nahdi, inafanya biashara katika nchi mbalimbali za Afrika, ikiwa ni pamoja na Tanzania, Zambia, Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi. Kwa uwekezaji huu mkubwa, kampuni hiyo inatarajiwa kuwa mzalishaji mkubwa zaidi wa saruji katika Afrika Mashariki, na kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya ujenzi na maendeleo ya miundombinu katika eneo hilo.