Katika hatua muhimu ya kuimarisha uchumi wa Zanzibar, Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Taasisi ya Fedha ya Ufaransa (BPI France) imetia saini mkataba wa kuikopesha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kiasi cha Euro milioni 37.5, ambacho ni sawa na takribani Shilingi Bilioni 115. Mkopo huu unalenga kufunga Mfumo wa Usimamizi na Usajili wa Taarifa za Ardhi (LARIS). CRDB itachangia Euro milioni 7.949 huku BPI France ikitoa Euro milioni 29.55.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika Ikulu Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, alisema ardhi ni rasilimali muhimu kwa maendeleo. Aliongeza kuwa Serikali imeamua kuimarisha usimamizi wake kwa njia ya kidijitali ili kuondoa changamoto zilizopo, hususan migogoro ya umiliki na mipaka.
"Serikali inaweka mazingira rafiki kwa kila mwananchi kunufaika na ardhi anayoimiliki. Baada ya kufunga mfumo huu wa LARIS, taarifa zote za umiliki na usimamizi wa ardhi zitapatikana kirahisi," alisema Dk. Mwinyi. Alisisitiza kuwa kumaliza migogoro ya ardhi kupitia mifumo ya kidijitali kutawapa wananchi fursa ya kutumia ardhi zao kama dhamana ya mikopo katika taasisi za fedha, jambo litakaloongeza kasi ya maendeleo.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Khadija Khamis Rajab, alibainisha kuwa mfumo huo utasaidia pia serikali katika utambuzi wa wamiliki wa ardhi na ukusanyaji wa kodi, akisema makusanyo ya kodi ya ardhi yataongezeka mara mfumo utakapokamilika.
CRDB Yafungua Fursa za Kifedha
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema mfumo wa LARIS utaleta mageuzi makubwa katika sekta ya ardhi Zanzibar kwa kuweka misingi imara ya usimamizi na umilikishaji kwa njia ya kidijitali. "Mradi huu utafungua fursa mpya za kifedha na kiuchumi kwani urasimishaji wa ardhi utajenga imani kwa taasisi za fedha kutoa mikopo," alisema Nsekela.
Nsekela aliongeza kuwa CRDB inaendeleza ushirikiano wa kimataifa ili kufanikisha miradi mikubwa nchini, akitaja ushiriki katika Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) na Reli ya Kisasa (SGR). Alibainisha kuwa Zanzibar pekee imepokea zaidi ya Sh. Bilioni 484 kupitia CRDB kwa miradi ya barabara, shule na Uwanja wa Ndege wa Pemba.
Katika ubunifu, Nsekela alitaja kwamba benki hiyo imetoa hatifungani za kijani na Samia Infrastructure Bond, pamoja na CRDB Al Barakah Sukuk, zilizokusanya fedha nyingi kwa ajili ya kuchochea maendeleo katika sekta za ujasiriamali, biashara, kilimo na utalii.
Makamu wa Rais wa BPI France, Alienor Daugreilh, alisema taasisi hiyo imeamua kushirikiana na Zanzibar kutokana na imani juu ya uimara wa uchumi wa visiwa hivyo, akiahidi kuendeleza ushirikiano katika miradi ya maendeleo.