Katika kile kinachoonekana kama kuamsha ari mpya ya utendaji na kuondoa mazoea katika sekta nyeti ya uzalishaji, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, ametoa maagizo mazito kwa watendaji wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, akiwataka kuachana na kasumba ya "kulialia" na badala yake waje na majibu ya kibiashara kwa changamoto za wakulima.
Waziri Chongolo ametoa rai hiyo kali jana jijini Dodoma, Makao Makuu ya Nchi, wakati wa kikao kazi cha kimkakati kilichomkutanisha na "vichwa" vya taasisi muhimu zinazobeba uhai wa kilimo nchini. Vigogo waliohudhuria ni pamoja na kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Bodi ya Chai Tanzania, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA), Bodi ya Mkonge Tanzania na Kampuni ya Mbolea Tanzania.
Kilimo si Jembe Tu, ni Hesabu za Pesa Akizungumza kwa utulivu lakini kwa msisitizo mkubwa, Waziri Chongolo alibainisha kuwa dhana ya kilimo nchini lazima ibadilike kutoka kuwa shughuli ya kujikimu na kuwa biashara kamili yenye ushindani. Aliwataka wakurugenzi hao kutumia taaluma zao "kusuka" mikakati endelevu itakayopanua wigo wa masoko ya mazao ya Watanzania ndani na nje ya mipaka.
"Sisi ndio wenye dhamana ya chakula na biashara ya nchi hii. Kilimo ni biashara, na biashara inahitaji mikakati, siyo maneno matupu. Hakikisheni mnaweka mipango madhubuti ya kuhakikisha sekta hii inazidi kuimarika na kumuingizia mkulima fedha mfukoni. Nisingependa kusikia malalamiko ya 'hali ngumu' wakati tuna jeshi la wataalam wa kutosha kwenye sekta hii wanaolipwa na serikali," alisisitiza Mhe. Chongolo.
Vita Dhidi ya Viwavi na Usalama wa Mazingira Katika kuhakikisha usalama wa mazao na afya za walaji, Waziri aliiagiza Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA) kuacha kufanya kazi kama kisiwa. Amewataka kujenga mahusiano ya karibu na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili kuwa na nguvu ya pamoja wakati wa dharura za milipuko au matumizi ya viuatilifu yanayoweza kuhatarisha afya ya binadamu na uoto wa asili.
Vilevile, kilio cha wakulima wa pamba kuhusu kushambuliwa na wadudu kimepata msikilizaji. Waziri Chongolo ameielekeza TPHPA kushirikiana bega kwa bega na Bodi ya Pamba Tanzania kutafuta "dawa" ya kudumu ya kudhibiti viwavi ambao wamekuwa wakiwaumiza wakulima wa zao hilo la "Dhahabu Nyeupe" kwa kushusha kiwango cha mavuno.
Mkonge Urejeshewe Hadhi Yake Kuhusu zao la Mkonge, ambalo kihistoria liliwahi kuifanya Tanzania kutambulika duniani, Waziri Chongolo ametoa agizo mahususi kwa Bodi ya Mkonge Tanzania. Ametaka mchakato wa kurejesha mali na majengo ya bodi hiyo ambayo yapo mikononi mwa watu au taasisi nyingine ufanyike haraka.
"Mkonge una soko kubwa sana duniani kwa sasa. Bodi lazima isimame imara, fuatilieni na mrejeshe mali zenu na majengo ili mpate nyenzo za kupanua shughuli za kilimo na biashara ya zao hili. Tunataka kuona Mkonge unarudi kwenye chati na kuchangia pato la taifa kama zamani," alieleza.
Kikao hicho cha Dodoma kinatafsiriwa kama sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha Sekta ya Kilimo inakua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, huku mkazo ukiwa kwenye kuongeza thamani na kutafuta masoko ya uhakika kwa wakulima.