"Wanaume Mashine" Wageuka Lulu Kanda ya Kaskazini: 70 Watawazwa 'Magwiji wa Jinsia', Wakubali Kubeba Watoto na Kupika

culture | Mon Dec 01 2025


"Wanaume Mashine" Wageuka Lulu Kanda ya Kaskazini: 70 Watawazwa 'Magwiji wa Jinsia', Wakubali Kubeba Watoto na Kupika

Katika kile kinachoonekana kama mapinduzi ya fikra na kuangusha ngome kongwe ya mfume dume, wanaume 70 kutoka mikoa ya Singida, Kilimanjaro na Arusha, wamevishwa taji la heshima na kutambulika rasmi kama 'Magwiji wa Usawa wa Kijinsia' (Gender Champions). Hatua hii imekuja baada ya wanaume hao kuamua kuweka kando mila na desturi zinazomkandamiza mwanamke na badala yake kushiriki kikamilifu katika kazi za nyumbani na malezi, jambo ambalo limewapa wake zao nafasi ya kupumua na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi.


Tukio hili la aina yake limejiri wakati wa Mkutano Mkuu wa 14 wa Mwaka wa Shirika la Maendeleo ya Jamii la TUSONGE CDO. Wanaume hawa, ambao sasa wamegeuka kuwa "taa na nuru" katika vijiji vyao, wamethibitisha kuwa uanaume si kukaa kijiweni kusubiri chakula, bali ni kushirikiana na mke katika kila hatua ya maisha, kuanzia jikoni hadi shambani.


Kuvunja Mwiko na Kujenga Umoja Akizungumza kwa hisia wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TUSONGE CDO, Bi. Aginatha Rutazaa, amesema shirika hilo limebadili mbinu za mapambano. Alibainisha kuwa kwa muda mrefu harakati za ukombozi wa mwanamke zililenga wanawake pekee, lakini sasa wamegundua kuwa "huwezi kupiga makofi kwa mkono mmoja."


"Mabadiliko ya kweli yanahitaji umoja wa dhati. Tumeona hatuwezi kufika tunapotaka kama tutawaacha wanaume nyuma. Hivyo, tumeweka nguvu kubwa kuhamasisha wanaume wenye nia njema, wale ambao wameelewa kuwa kumsaidia mke si udhaifu, bali ni uimara wa familia," alisema Bi. Rutazaa na kuongeza:


"Ndani ya kipindi hiki, tumefanikiwa kuwapata wanaume 70 jasiri waliopitia mafunzo yetu. Hawa wamekuwa chachu ya mabadiliko katika jamii za Kanda ya Kaskazini na Kati. Wameitikia wito wa kushiriki malezi na majukumu ya nyumbani, na sisi tumewapa heshima ya kuitwa 'Gender Champions'. Wanafanya kazi kubwa sana ya kuelimisha wenzao vijiweni."


Samaki Mkunje Angali Mbichi: Mradi Mpya Mashuleni Mbali na kuwapongeza wanaume hao, TUSONGE CDO imetangaza mkakati mpya wa kuandaa kizazi kijacho. Bi. Rutazaa amebainisha kuwa wamekuja na mradi wa kuanzisha 'Klabu za Uongozi na Uchumi' katika shule za msingi, wakilenga zaidi madarasa ya chini (Darasa la Pili na la Tatu).


Falsafa nyuma ya mradi huu ni kuziba pengo la uongozi na uchumi ambalo limekuwa likigharimu taifa. Imebainika kuwa vipaji vingi hupotea kwa sababu watoto hawajengewi misingi ya kujiamini na kujitegemea kiuchumi wangali wadogo.


Uchumi na Uongozi: Kama Mgonjwa na Uji Akifafanua zaidi kuhusu uhusiano wa uongozi na uchumi, Mkurugenzi huyo alitumia msemo wa kiswahili unaosema vitu hivyo ni kama "mgonjwa na uji," akimaanisha havitenganishwi.


"Tumegundua kuwa huwezi kuwa kiongozi bora kama huna uhuru wa kiuchumi. 'Economic Empowerment' au Uwezeshaji wa Kiuchumi ndiyo nguzo inayompa mtu sauti na mamlaka. Bila fedha au uwezo wa kuzalisha, uongozi unakuwa dhaifu. Hivyo, tunataka watoto hawa wakue wakijua kuwa uongozi na uchumi vinakwenda sambamba, havitengamani," alisisitiza.


Hatua hii ya TUSONGE inatazamwa kama mwarobaini wa changamoto nyingi za kijamii, ikijenga familia imara ambapo baba na mama wanashirikiana, huku ikiandaa kizazi cha kesho kinachojitambua kiuchumi na kiuongozi. Wanaume hawa 70 sasa wanabeba dhamana ya kuwa mabalozi wa kueneza injili hii ya usawa katika maeneo ambayo mfume dume bado umetamalaki.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.