Wazazi na walezi mkoani Mtwara wamepewa wito wa kuwapa watoto wa kike na watoto wenye mahitaji maalum fursa za kupata mafunzo ya ufundi stadi ili kuwasaidia kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Chuo cha VETA Mkoa wa Mtwara, Bi. Theresia Ibrahim, alipokuwa akihitimisha mafunzo ya vijana 69, ambapo kati yao wanaume walikuwa 54 na wanawake 15. Mafunzo hayo yaliandaliwa na Shirika la ADEA kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kusini Mashariki, Bi. Ibrahim alisema kuwa bado kuna dhana potofu iliyojengeka miongoni mwa jamii kwamba watoto wa kike na watoto wenye mahitaji maalum hawawezi kujifunza na kushiriki katika fani mbalimbali za ufundi stadi.
“Katika mafunzo haya, wanawake ni wachache sana, na pia nimeona kijana mmoja tu mwenye mahitaji maalum. Wazazi na walezi tunapaswa kuwawekeza kwa watoto hawa. Sio kwamba hawawezi, bali wanahitaji kupewa fursa na kuhamasishwa kushiriki kwenye mafunzo haya ili waweze kujitegemea,” alisema Bi. Ibrahim kwa msisitizo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la ADEA, Bwana Saidi Chilumba, alibainisha kuwa moja ya changamoto kubwa waliyokutana nayo ni idadi ndogo ya wasichana wanaojiunga na mafunzo hayo, hali ambayo inasababishwa na mitazamo ya familia pamoja na uhaba wa wakufunzi wa lugha za alama kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa kusikia.
“Natoa wito kwa vijana wa kike wasikubali kukatishwa tamaa. Wawe na ujasiri wa kujiamini na kujiendeleza katika fani zao,” alisema Bwana Chilumba. Aliwasihi pia wazazi na walezi kuwapa watoto wa kike na wenye mahitaji maalum fursa sawa na watoto wengine katika kupata elimu na mafunzo ya ufundi.
Mafunzo hayo yalihusisha fani mbalimbali kama vile uchongaji, uchoraji, useremala, na ufundi chuma. Wahitimu wa mafunzo hayo wanatarajiwa kutumia ujuzi waliopata kuongeza thamani ya bidhaa wanazotengeneza na kujiongezea kipato, na hivyo kuboresha maisha yao na kuchangia katika maendeleo ya jamii.
Mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, Bi. Asfa Rashidi, alishukuru Shirika la ADEA kwa kutoa mafunzo hayo. Alisema kuwa mafunzo hayo yatakuwa msaada mkubwa kwa vijana wengi katika kuboresha maisha yao kupitia ujuzi wa ufundi stadi. Aliongeza kuwa ujuzi walioupata utawawezesha kujiajiri na kuondokana na utegemezi.
Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi na kuhakikisha kuwa kila mtu, bila kujali jinsia yake au hali yake ya kiafya, anapata nafasi sawa ya kushiriki katika maendeleo ya jamii.