Kutoka Kwenye Aibu Hadi Ujasiriamali: Simulizi ya Saraphina Yazindua Mradi Mpya wa SOS Iringa

culture | Mon Apr 14 2025


Kutoka Kwenye Aibu Hadi Ujasiriamali: Simulizi ya Saraphina Yazindua Mradi Mpya wa SOS Iringa

Katika Kijiji cha Kiwele, Wilayani Iringa, maisha ya Saraphina Sanga ni ushuhuda hai wa nguvu ya mabadiliko na kupata fursa ya pili. Akiwa msichana wa miaka 17 tu, tayari alikuwa amebeba jukumu la ulezi, ndoto zake zikiwa zimezimika ghafla baada ya kupata ujauzito. Alijawa na aibu, akakosa uhuru na kujiona hana thamani tena mbele ya jamii, kiasi cha kuishi kwa kujificha. Matumaini ya kesho yalikuwa yamepotea kabisa.


Hata hivyo, kupitia mradi wa awali wa "Watoto Wenye Watoto" ulioendeshwa na Shirika la SOS Children’s Villages Tanzania mkoani Iringa, Saraphina alipata mwanga mpya. Alifundishwa kuhusu malezi chanya, akapatiwa stadi za ujasiriamali, na kupata maarifa muhimu kuhusu afya ya uzazi. Leo, Saraphina ni mtu tofauti kabisa – mwanamke kijana aliyejaa kujiamini, anayetambua haki zake, na mwenye ndoto kubwa kwa ajili yake na mtoto wake.


“Kabla ya kuingia kwenye mradi, nilikuwa siwezi hata kuongea mbele ya watu, hata wanawake wenzangu. Nilihisi maisha yangu yamekwisha nilipopata mimba,” anasimulia Saraphina kwa utulivu, huku tabasamu la ushindi likichanua usoni mwake. "Lakini sasa, najiamini kuzungumza, nina biashara zangu ndogondogo, na nimekuwa mshauri kwa wasichana wengine hapa kijijini wasikate tamaa na ndoto zao."


Simulizi hii ya kusisimua ya Saraphina imekuwa chachu na kiini cha matumaini wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi mpya wa miaka mitatu unaojulikana kama "Mradi wa Kuwezesha Vijana katika Afua za Afya ya Uzazi na Uchumi Endelevu". Mradi huu unalenga kuwafikia wasichana waliopata watoto katika umri mdogo na wale wanaoishi katika mazingira magumu, pamoja na vijana wa kike na kiume walio katika umri balehe.



Mradi huu utakaotekelezwa katika wilaya za Mufindi na Kilolo mkoani Iringa, unafadhiliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland kupitia SOS Children’s Villages Tanzania. Madhumuni yake makuu ni kuboresha ustawi wa vijana, kukuza usawa wa kijinsia, kupiga vita ukatili wa kijinsia, kupunguza umasikini, na kuongeza uelewa kuhusu afya ya uzazi. Unatarajiwa kuwafikia vijana wapatao 30,000 na kuwawezesha kiuchumi takriban kinamama 300 waliopata watoto katika umri mdogo.


Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi, Naibu Mkurugenzi wa Kitaifa wa SOS Children’s Villages Tanzania, Bi. Doroth Ndege, alieleza kuwa mafanikio ya miradi ya awali, kama ule uliomsaidia Saraphina, yametoa msingi thabiti. "Uzoefu wetu na ushahidi wa mabadiliko chanya kama ya Saraphina vinatupa uhakika kuwa kuwekeza katika elimu, afya, na ustawi wa kijinsia kwa vijana kunaleta matokeo halisi," alisema Bi. Ndege.


Aliongeza kuwa mradi huu ni mwendelezo wa juhudi za shirika hilo za zaidi ya miaka 30 nchini Tanzania katika kutoa malezi mbadala na kuwawezesha vijana, hasa wasichana ambao ndoto zao zilikatishwa na ujauzito wa mapema. "Tunataka kuona wasichana hawa wakiamka tena, wakijiamini na wakishiriki kikamilifu katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii zao," alisisitiza. Mradi huu pia umezingatia mafunzo yaliyopatikana kutokana na tathmini za mradi wa "Watoto Wenye Watoto" (2021-2023) ili kuhakikisha unaenda kukidhi mahitaji halisi ya walengwa, huku ukijumuisha watu wenye ulemavu na kupambana na unyanyapaa.


Shirika la SOS Children’s Villages limekuwa likitoa huduma nchini tangu 1991 na linafanya kazi katika mikoa saba ikiwemo Iringa (tangu 2016), ambapo limefikia zaidi ya vijana 20,000 na kaya 500 kupitia programu mbalimbali. Lengo kuu la shirika ni kufikia wanufaika milioni 2.5 ifikapo 2028.


Akizindua mradi huo kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Katibu Tawala Msaidizi Bi. Nuru Sovela, aliipongeza SOS kwa mradi huo na kusisitiza kuwa serikali inathamini mchango wa wadau katika maendeleo ya vijana. "Tumevutiwa sana na shuhuda hizi za mabadiliko. Tunahitaji kupata taarifa za utekelezaji kila baada ya miezi mitatu ili tufuatilie kwa karibu na kuhakikisha uendelevu," alisema Bi. Sovela.



The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.