Tangu kupata uhuru wake, Tanzania imekuwa ikipambana vikali na magonjwa mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kutimiza azma ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyetangaza ujinga, maradhi, na umaskini kuwa maadui wakuu wa nchi. Serikali zote zilizofuata zimeendeleza vita hii kwa juhudi kubwa. Hivi karibuni, taifa limefanikiwa kupiga hatua muhimu katika kupunguza maambukizi mapya ya Kifua Kikuu (TB).
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani kwa mwaka 2025, yaliyofanyika jijini Arusha, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, alitangaza kuwa maambukizi ya TB yamepungua kwa kiasi kikubwa. Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2015, kulikuwa na wagonjwa 306 kwa kila watu 100,000. Hata hivyo, kufikia mwaka 2023, idadi hiyo imepungua hadi kufikia wagonjwa 183 kwa kila watu 100,000. Hii ni sawa na upungufu wa asilimia 40 ndani ya kipindi hicho.
Dkt. Mollel alifafanua kuwa mafanikio haya yameweka Tanzania katika orodha ya nchi 13 duniani ambazo zinaelekea kutimiza malengo ya kimataifa ya kupunguza maambukizi mapya ya TB kwa asilimia 50 na vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2025. Aliongeza kuwa Tanzania inaelekea vizuri katika azma yake ya kutokomeza kabisa ugonjwa wa Kifua Kikuu ifikapo mwaka 2030, kwa mujibu wa malengo endelevu ya Umoja wa Mataifa.
Sambamba na kupungua kwa maambukizi, Dkt. Mollel alibainisha kuwa vifo vinavyotokana na TB navyo vimepungua kwa kiwango kikubwa. Takwimu zinaonyesha kuwa kulikuwa na vifo 56,000 mwaka 2015, lakini idadi hiyo ilishuka hadi vifo 18,400 mwaka 2023, ikiwa ni punguzo la asilimia 68. Mafanikio haya yanadhihirisha ufanisi wa mikakati inayotekelezwa na serikali katika kukabiliana na ugonjwa huu hatari.
Ni dhahiri kuwa serikali inastahili pongezi kwa hatua hizi muhimu, ambazo ni sehemu ya utekelezaji wa ndoto za Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, na viongozi wengine waliofuata, akiwemo Rais wa sasa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuweka afya ya wananchi kuwa kipaumbele.
Mafanikio haya yanatokana na juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na serikali katika kuboresha huduma za Kifua Kikuu nchini. Hii ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi na upimaji wa ugonjwa huo katika vituo vingi vya afya, hasa katika ngazi za jamii. Pia, serikali imekuwa ikishirikisha jamii kwa karibu kupitia kampeni mbalimbali za uhamasishaji zinazolenga kuongeza uelewa kuhusu TB na umuhimu wa kutafuta matibabu mapema.
Kampeni hizi zimekuwa zikihamasisha jamii na wadau mbalimbali kuhusu wajibu wao katika kuchangia jitihada za kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini. Ni muhimu juhudi hizi ziendelee kwa kasi zaidi ili kufikia lengo la kutokomeza kabisa ugonjwa huu na magonjwa mengine yanayoathiri afya ya wananchi kabla ya mwaka 2030.
Zaidi ya hayo, kuna umuhimu wa kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu dalili za ugonjwa wa Kifua Kikuu, ili watu wenye dalili waweze kutafuta matibabu mapema. Kutafuta matibabu mapema ni muhimu sana katika kuzuia kuenea kwa maambukizi mapya katika jamii na kupunguza hatari ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huu.
Tunafahamu kuwa kuna kampeni inayoendelea katika halmashauri 76 za mikoa tisa kwa lengo la kuwatambua wagonjwa wa Kifua Kikuu na kuwaanzishia tiba. Kampeni hii, inayoendeshwa na wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ilianza Desemba 2024 na inatarajiwa kumalizika Machi 2025. Mafanikio yaliyopatikana kupitia kampeni hii ni ya kutia moyo, ambapo tayari wagonjwa 9,585 wa Kifua Kikuu wamegunduliwa na wameanza kupata matibabu, ikiwa ni sawa na asilimia 66 ya lengo la kutambua wagonjwa 14,471.
Hatua hizi zote zinatufanya tuipongeze serikali kwa dhati na kushauri vita hii dhidi ya Kifua Kikuu iendelee kwa nguvu ili kuepusha madhara yanayotokana na wananchi kuugua, ikiwemo kupoteza nguvu kazi muhimu kwa maendeleo ya taifa. Ni muhimu kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anaishi maisha yenye afya bora na anaweza kuchangia katika kujenga uchumi imara wa nchi.