Matokeo ya Mashindano ya Kitaifa ya Hisabati (TAMO) kwa mwaka 2025 yametangazwa na Chama cha Hisabati Tanzania (MAT/CHAHITA), huku picha ikionesha wazi jinsi wanafunzi wa kiume walivyong'ara na kutawala alama za juu, na kuwaacha wanafunzi wa kike nyuma katika nyanja hiyo muhimu kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini.
Akitangaza matokeo hayo jijini Dodoma, Mwenyekiti wa CHAHITA, Dk. Said Sima, alifafanua kuwa jumla ya wanafunzi 1,736 kutoka kidato cha tatu hadi cha sita walishiriki kutoana jasho katika mtihani huo uliofanyika Agosti 8, 2025. Mashindano haya, ambayo ni muhimu kwa ajili ya kuibua na kukuza vipaji vya hisabati, yaliandaliwa kwa ushirikiano wa karibu na Idara ya Hisabati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kudhaminiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Uchambuzi wa kina unaonesha kuwa katika kundi la wanafunzi 1,117 wa kidato cha tatu na nne, ni 172 pekee waliovuka alama ya asilimia 40. Kati ya kundi hili la waliofaulu vizuri, wavulana walikuwa 112, sawa na asilimia 65 ya waliofanya vizuri zaidi, huku wasichana wakiwa 60 tu, ambayo ni asilimia 35. Hali hii inadhihirisha pengo kubwa la ufaulu kati ya jinsia hizi katika somo la hisabati.
Katika kundi hili, Goodluck Lyali kutoka Shule ya Sekondari Ilboru, Arusha, aliibuka kinara wa kitaifa, akifuatiwa na majina mengine ya wavulana kama Yohana Nsila wa Mzumbe (Morogoro), na Silvanus Alfred pamoja na Mikidadi Misai kutoka Marian Boys (Pwani). Kwa upande wa wasichana, Nasra Shabani wa St. Monica Girls (Arusha) na wanafunzi kutoka shule maarufu kama St. Francis Girls (Mbeya) na Feza Girls (Dar es Salaam) waliongoza kundi lao.
Hali haikuwa tofauti kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita. Kati ya washiriki 619, wavulana walitawala tena kwa kiasi kikubwa kundi la waliofaulu kwa alama zaidi ya asilimia 40. Kwenye kundi la ufaulu wa kati (asilimia 20-39), wavulana walichukua asilimia 75 ya nafasi zote. Mwanafunzi Zacharia Mwita, pia kutoka Ilboru (Arusha), aliongoza kundi hili, akifuatiwa na Henry Rulagirwa wa Tabora Boys. Majina ya wasichana waliofanya vizuri yalitoka katika shule kama Msalato (Dodoma), Lumumba (Zanzibar), na Kilakala (Morogoro).
Dk. Sima alisisitiza kuwa lengo kuu la mashindano haya ya kila mwaka si tu kutambua vipaji, bali pia kuongeza hamasa na ari ya kujifunza hisabati, somo ambalo ni uti wa mgongo wa fani nyingi. Aliongeza kuwa washindi hawa ndio watakaounda timu ya taifa itakayopeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano ya kimataifa ya hisabati.