Ilikuwa ni safari ya kukata tamaa alfajiri na mapema. Kwenye barabara ya vumbi, Paulo alikanyaga pedeli za baiskeli yake kwa nguvu, huku nyuma mkewe, Anna, akivuja jasho na kulia kwa uchungu wa kujifungua. Hakuwa na mimba ya kawaida; alikuwa akielekea kujifungua mapacha watatu. Huu ulikuwa mwanzo wa kisa cha kushangaza cha uhai na kifo katika kijiji cha Genge Sita, Wilaya ya Uyui, ambacho kimebaki kuwa ushahidi hai wa umuhimu wa mradi wa "Jamii Salama" wa Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete (JMKF).
Genge Sita ni kijiji kilichosahaulika, umbali wa kilomita 14 kutoka zahanati ya karibu. Miezi michache kabla ya safari hiyo ya baiskeli, timu ya mradi wa Jamii Salama, unaolenga kupeleka huduma za afya ya mama na mtoto vijijini, ilifika kijijini hapo. Miongoni mwa waliojitokeza alikuwa Anna, mwenye ujauzito wa miezi saba. Vipimo vyao vya 'ultra sound' na shinikizo la damu vilionesha hatari: mama huyu alikuwa na shinikizo la damu la juu na alibeba mapacha watatu, jambo ambalo hakulijua. Timu ilimpa dawa, elimu, na rufaa yenye msisitizo: "Kujifungua hospitali kubwa."
Hata hivyo, umasikini na ukosefu wa usafiri uliwazuia. Mnamo Juni 10, uchungu ulipomshika, baiskeli ndiyo ilikuwa tegemeo lao. Safari haikufika mbali. Kijiji cha jirani, Anna alizimia. Walipokelewa na msamaria mwema, na kwa msaada wa kijana aliyesomea ufamasia, Anna alijifungua watoto watatu—mvulana na wasichana wawili—juu ya sakafu ya udongo.
Furaha ya uzazi iligeuka hofu haraka. Anna alianza kutikisika, akipatwa na kifafa cha uzazi (eclampsia), hali inayoweza kuua. Maisha yake yalining'inia. Kijana aliyewasaidia aliwasiliana na timu ya Jamii Salama. Majaribio ya kupata gari la wagonjwa kupitia mfumo rasmi wa dharura wa M-Mama yalikwama. Hapo ndipo ubinadamu uliposhinda urasimu. Timu ya Jamii Salama haikusita; walimbeba Anna kwenye gari lao binafsi na kukimbia naye hospitali ya mkoa, wakimpa huduma ya kwanza njiani.
Hospitalini, Anna alipatiwa damu na huduma za dharura zilizookoa maisha yake. Watoto wake, ingawa dhaifu, walikuwa salama. Ushindi huu ulikuwa wa wengi: familia, kijana shujaa, na hasa mradi wa Jamii Salama. Kwa shukrani, wazazi waliwapa watoto wao majina yenye maana: mvulana aliitwa Jakaya kwa heshima ya mwanzilishi wa JMKF; msichana wa kwanza akaitwa Marcelina, jina la mratibu wa mradi aliyesisitiza umuhimu wa rufaa; na mdogo wao akaitwa Shija, jina la Kisukuma lenye maana ya mtoto wa tatu kuzaliwa.
Kisa hiki ni sehemu ndogo ya mafanikio ya mradi uliogusa maisha ya wanawake zaidi ya 1,500 ndani ya miezi minne katika wilaya za Uyui na Sikonge. Mradi huu umethibitisha kuwa kupeleka huduma karibu na wananchi sio tu sera nzuri, bali ni njia ya uhakika ya kushinda kifo na kuleta matumaini pale yalipopotea.