Upepo wa mabadiliko katika shughuli za mapishi umeanza kuvuma jijini Dar es Salaam, ambapo wananchi wanaendelea kupata elimu na hamasa kuhusu mapinduzi ya matumizi ya nishati safi ya umeme jikoni. Hii ni sehemu ya Kampeni kabambe ya Kitaifa ya Uhamasishaji wa Upishi wa Umeme (eCooking), iliyozinduliwa rasmi na serikali Juni 13, 2025.
Kampeni hii, inayoendeshwa na Wizara ya Nishati kwa ushirikiano na washirika wa maendeleo ikiwemo Programu ya Huduma za Nishati za Kisasa za Kupikia (MECS) na Shirika la Maendeleo la Uingereza (UK International Development), inalenga moja kwa moja kubadili maisha ya mamilioni ya Watanzania. Lengo kuu ni kuzinusuru kaya na athari za kiafya na kimazingira zinazosababishwa na utegemezi wa muda mrefu wa nishati ya kuni na mkaa.
Inafahamika wazi kuwa matumizi ya kuni na mkaa, mbali na kuchangia uharibifu wa misitu, husababisha magonjwa ya mfumo wa hewa na matatizo ya macho, hasa kwa wanawake na watoto wanaotumia muda mwingi jikoni. Kampeni ya eCooking inakuja na suluhisho la kudumu la kuondokana na adha hizi kwa kutoa njia mbadala iliyo safi, salama na rafiki kwa mazingira.
Ili kuhakikisha ujumbe unafika kote nchini, kampeni imepata nguvu mpya baada ya washirika wa maendeleo kuikabidhi Wizara ya Nishati magari mawili mapya. Magari haya yatatumika kama vituo vya elimu vinavyotembea, vikizunguka maeneo mbalimbali, kuanzia Dar es Salaam, kutoa elimu, kufanya maonesho ya vifaa vya upishi wa umeme, na kufuatilia maendeleo ya kampeni. Ni hatua muhimu itakayohakikisha hata wananchi wa maeneo ya mbali wanafikiwa na teknolojia hii ya kisasa.