Serikali katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, imetangaza vita dhidi ya kero ya kelele za usiku, ikipiga marufuku shughuli zote za muziki wa sauti ya juu kutoka kumbi za starehe na hata nyumba za ibada baada ya saa sita usiku. Hatua hiyo imechukuliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Frank Nkinda, kufuatia malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi wanaokosa usingizi na kushindwa kupumzika.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya maegesho ya malori katika Kata ya Majengo, Nkinda alisema uhuru wa kufanya biashara au kuabudu haupaswi kuwa adhabu kwa wengine. Alieleza kuwa amepokea malalamiko mengi kuhusu kumbi za burudani na baadhi ya madhehebu ya dini yanayokesha na ibada zenye kelele za vyombo vya muziki hadi majogoo, na kusababisha usumbufu mkubwa.
"Haiwezekani watu washindwe kupumzika majumbani mwao kwa sababu ya biashara ya mtu mwingine au ibada. Haki ya kupumzika ni ya msingi," alisema Nkinda. "Natoa agizo, mwisho wa kupiga muziki kwa sauti ya juu iwe ni saa sita kamili za usiku. Hii inajumuisha kumbi zote za starehe na madhehebu ya kilokole. Punguzeni sauti za vyombo vyenu."
Agizo hilo limekuja kama faraja kwa wakazi wengi, akiwemo Mustapha Mayala kutoka Kata ya Majengo. Mayala alieleza kuwa kelele hizo zimekuwa na madhara makubwa, ikiwemo kuwafanya wanafunzi washindwe kujisomea usiku na hata kuhatarisha afya za wagonjwa, hasa wenye shinikizo la damu (presha).
Ili kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa kikamilifu, Mkuu huyo wa Wilaya amemuagiza Ofisa Utamaduni wa Manispaa ya Kahama kusimamia zoezi hilo kwa ukamilifu na bila upendeleo. Alisisitiza kuwa yeyote atakayekiuka sheria hiyo, awe mmiliki wa ukumbi wa starehe au kiongozi wa dini, atachukuliwa hatua kali za kisheria.
"Ofisa Utamaduni, hakikisha hii kero inakoma. Simamia sheria na yeyote atakayekwenda kinyume achukuliwe hatua. Wananchi wanahitaji kupumzika ili kesho yake waweze kushiriki katika ujenzi wa taifa," alihitimisha Nkinda.