Mwalimu Mkuu Akamatwa Shinyanga kwa Kumshushia Kipigo Kingi Mwanafunzi wa Darasa la Saba

culture | Sat May 17 2025


Mwalimu Mkuu Akamatwa Shinyanga kwa Kumshushia Kipigo Kingi Mwanafunzi wa Darasa la Saba

Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga linamshikilia Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ngilimba, iliyopo Kata ya Ulowa, Halmashauri ya Ushetu, Erick Ombeni, akituhumiwa kumpiga mwanafunzi wa darasa la saba, Julius Paul (mwenye umri wa miaka 15), na kumuachia majeraha makubwa mwilini. Tukio hili la kusikitisha lilitokea tarehe 14 Mei, mwaka huu, asubuhi wakati wa mtihani wa majaribio (moko).


Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, mwanafunzi huyo alipata vipigo katika sehemu mbalimbali za mwili wake, huku akijeruhiwa zaidi eneo la mgongo. Kamanda Magomi amethibitisha kuwa uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini ukweli wote wa tukio hilo kabla ya kumfikisha mtuhumiwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili. Uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha adhabu hiyo kinadaiwa kuwa mwanafunzi huyo alifanya makosa ya kufutafuta jina lake kwenye karatasi ya majibu wakati wa mtihani.


Mama mzazi wa Julius, Bi. Pauline Benedicto, amesimulia kwa uchungu jinsi alivyomkuta mwanae akilia njiani asubuhi ya siku ya tukio, akiwa anampelekea chakula. Alipomuuliza nini kimempata, Julius alianguka chini kutokana na maumivu. Baada ya kumbeba hadi nyumbani, mwanafunzi huyo alimsimulia jinsi Mwalimu Mkuu alivyomshambulia kwa kiboko. Mama huyo alitoa taarifa kwa viongozi wa serikali za kijiji na kata.


Aliongeza kuwa kutokana na hali mbaya ya mwanae, waliandikiwa barua kwenda zahanati kwa matibabu ya awali huku wakimsubiri Mwalimu Mkuu afike ofisi za kata kuzungumzia suala hilo. Hata hivyo, Mwalimu hakuweza kufika kwa wakati kwa madai alikuwa akisimamia mitihani. Walipofika shuleni, Mwalimu Mkuu alikiri kumpiga mtoto huyo akidai alikosea mara kadhaa kwenye karatasi ya majibu, na alifanya hivyo kwa hasira, akaomba radhi kwa kitendo hicho cha kupitiliza.


Akisimulia kwa upande wake, mwanafunzi Julius ameeleza kuwa alikosea kuandika jina lake kwenye karatasi ya mtihani, jambo lililopelekea ikachafuka. Mwalimu Mkuu alimsimamisha mbele ya wanafunzi wenzake na kumtaka aandike jina ubaoni huku akimtandika viboko sehemu mbalimbali za mwili wake.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngilimba, Ndugu Zuberi Mabula, ameeleza kuwa baada ya kupokea malalamiko hayo, walimshauri Mwalimu Mkuu kukutana na familia na kusaidia matibabu ya mtoto, lakini Mwalimu hakuonesha ushirikiano, hivyo waliamua kuripoti tukio hilo polisi kwa hatua za kisheria.


Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama, Andrew Chatwanga, amelaani vikali tukio hilo akisema kitendo hicho si cha kiungwana na hakiwezi kuvumiliwa. Amesisitiza kuwa mwanafunzi amepata majeraha makubwa hata kichwani, hali ambayo ni hatarishi.


Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mheshimiwa Emmanuel Cherehani, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara kijijini hapo, ameahidi kumsaidia mwanafunzi huyo kupata matibabu stahiki ili aweze kupona na kuendelea na masomo yake, hasa ikizingatiwa yuko darasa la saba ambalo ni la mitihani ya taifa. Pia ameliomba jeshi la polisi kukamilisha upelelezi haraka na kuchukua hatua zinazostahili.


Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa Waraka wa Elimu namba 24 wa mwaka 2002, adhabu ya viboko shuleni inapaswa kutolewa na Mwalimu Mkuu au mwalimu aliyepewa kibali kwa maandishi, isizidi viboko vinne kwa kosa moja la jinai au la kinidhamu. Tukio hili linaibua tena mjadala kuhusu matumizi ya adhabu ya viboko shuleni na athari zake kwa wanafunzi.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.