Wanafunzi na watoto walio chini ya umri wa miaka 18 katika wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera, wamepewa uhakikisho kamili kuwa siri zao zitahifadhiwa wanapotoa taarifa kuhusu ukatili wanaokumbana nao shuleni na majumbani. Ahadi hii imetolewa ili kuondoa hofu na kuwawezesha watoto kutoa taarifa bila wasiwasi wa vitisho kutoka kwa wahalifu.
Timu ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) ilikutana na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Minziro, inayochukua wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita. Katika mkutano huo, wanafunzi walipata elimu ya kisheria kuhusu ukatili wa kijinsia na mbinu sahihi za kufikia mamlaka husika ili kuhakikisha changamoto zao zinasikilizwa, siri zao zinatunzwa, na wahalifu wanachukuliwa hatua za kisheria.
Grace Matofali, kutoka Dawati la Jinsia la Kitengo cha Polisi Missenyi, ambaye pia ni miongoni mwa wataalamu wanaotoa elimu ya msaada wa kisheria, alieleza kwa kina madhara ya ukatili kwa jamii na changamoto zinazowakumba wanafunzi. Alisema kuwa kuna wimbi la wahalifu wanaowatisha watoto waliobakwa na kulawitiwa, wakitishia kuwaua iwapo watafichua matendo hayo. Hali hii imekuwa ikisababisha hofu kubwa kwa watoto.
“Kwa upande wa polisi, tunapokea takribani kesi tano au sita za ubakaji na ulawiti, na idadi kubwa zaidi ya kesi za vipigo, ambazo zinaweza kuzidi hata hamsini kwa mwezi. Lakini kuna kundi la wahalifu wanaotumia vitisho. Mhalifu anambaka mtoto, kisha anamwambia akisema, ‘Nitakuua, nitakunyonga.’ Ninawaomba niwahakikishie kuwa serikali imeweka ulinzi mkubwa kwa watoto, hivyo waondoe hofu,” alisema Grace Matofali.
Hakika Ibrahim, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Missenyi, alithibitisha kuwa wilaya hiyo inapokea kati ya kesi hamsini hadi sitini kwa mwezi zinazohusu masuala mbalimbali ya ukatili dhidi ya watoto. Alisema malalamiko mengi yanahusu utekelezaji mbaya wa wazazi, mimba za utotoni, ubakaji, na ulawiti, ambayo ni changamoto kubwa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18.
Aliongeza kuwa serikali kwa sasa imejikita sana katika kuwashughulikia wahalifu wanaotenda matukio ya ukatili dhidi ya watoto, wakiwemo wanafunzi. Alitoa mfano wa hivi karibuni ambapo baba mmoja alihukumiwa kifungo cha miaka 30 kwa kumpa mimba mtoto wake. Pia, alidai kuwa serikali ya Missenyi imefanikiwa kumrejesha mwanafunzi mmoja shuleni na kumpeleka kidato cha kwanza baada ya wazazi wake kumtorosha ili kumpeleka wilaya ya Rongido kufanya kazi. Kutokana na hatua hizi, aliwahimiza watoto wasiogope kutoa taarifa za ukatili.