Wakati dunia ikijiandaa kuwasha mishumaa ya maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya limeamua kutolala usingizi na badala yake "kupeleka moto" mashuleni ili kuwanoa vijana kujitambua na kukataa kuwa wahanga wa vitendo vya kikatili.
Katika kile kilichoonekana kama operesheni ya "Okoa Kizazi Chetu", Maafisa waandamizi wa Jeshi hilo wametua katika Shule ya Sekondari ya Mbeya Day (Mbeya Day Secondary School) iliyopo katikati ya jiji la Mbeya, na kutoa elimu ambayo imetajwa kuwa ni 'chanjo' dhidi ya mmomonyoko wa maadili.
ASP Panera: "Vunjeni Ukimya, Fichueni Wahalifu" Akizungumza kwa sauti ya kiamri na yenye uchungu wa kibmzazi mbele ya mamia ya wanafunzi Desemba Mosi, 2025, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mbeya, ASP Veronica Panera, amesema muda wa "kufunika kombe mwanaharamu apite" umekwisha. ASP Panera amebainisha kuwa vitendo vya aibu kama ubakaji, ulawiti na vipigo bado vinatafuna jamii kwa siri, na dawa pekee ni wanafunzi kuwa majasiri wa kusema "BASI".
"Tumekuja hapa kutekeleza kampeni maalum. Hatuwezi kufumbia macho vitendo vya kinyama wanavyofanyiwa watoto wetu. Nawaagiza ninyi wanafunzi, msiogope vitisho vya wahalifu. Mkimuona mtu anataka kuwafanyia ukatili au amewafanyia, pigeni kelele, ripoti polisi, ripoti kwa walimu. Sheria imunoa makali na itachukua mkondo wake bila kumuonea haya mtu," alisisitiza ASP Panera.
SP Mahenge na "Ugonjwa" wa Tamaa Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Mbeya, SP Nuru Mahenge, aligusa mzizi wa fitina unaowaponza wanafunzi wengi; tamaa ya vitu vidogo. Alitumia lugha ya vijana kuwatahadharisha dhidi ya kupenda "dezo" kama lifti za magari ya watu wasiowajua, chipsi, na zawadi ndogondogo ambazo mara nyingi huwa ni chambo cha kuwanasa katika mitego ya ukatili.
"Epukeni makundi hatarishi yanayowashawishi kutoroka shule au kujihusisha na mapenzi katika umri mdogo. Tamaa ya vitu vidogo ndiyo mlango wa kuingia kwenye matatizo makubwa. Jikubalini na ridhikeni na kile wazazi wenu wanachowapa," alishauri SP Mahenge.
CARE International na Vita ya Kidijitali Wadau wa maendeleo nao hawakuachwa nyuma. Mratibu wa Shirika la CARE International, Bw. Mwanane Madebo, ameeleza kuwa shirika hilo limeungana mkono na serikali kutoa elimu hiyo kwa makundi mbalimbali wakiwemo madereva wa vyombo vya moto na walimu.
Bw. Madebo alitanua wigo wa mjadala kwa kugusia madhara ya ukatili ambayo ni pamoja na vifo, ulemavu wa kudumu, na msongo wa mawazo unaoweza kuharibu ndoto za mwanafunzi. Aidha, alikumbushia kaulimbiu ya mwaka huu inayosema, “Ungana kutokomeza unyanyasaji wa kidijitali dhidi ya wanawake na wasichana wote,” akionya juu ya matumizi mabaya ya simu na mitandao ya kijamii yanayoweza kugeuka kuwa uwanja mpya wa udhalilishaji.
Ziara hii katika shule ya Mbeya Day ni sehemu ya mkakati mpana wa Mkoa wa Mbeya kuhakikisha elimu ya ukatili inawafikia walengwa mahali walipo kabla madhara hayajatokea.