Wito umetolewa kwa jamii, sekta binafsi, na wadau wote wa elimu nchini kuwekeza nguvu katika kujenga utamaduni thabiti wa usomaji, huku mkazo maalum ukiwekwa kwenye usomaji wa kidijitali ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani. Wito huo ulitolewa na Mdhibiti Ubora Mkuu wa Shule wa Manispaa ya Temeke, Lilian Kazenga, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Usomaji yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Kilamba jijini Dar es Salaam.
Kazenga alisisitiza kuwa jukumu la kumjengea mtoto tabia ya kupenda vitabu linaanzia nyumbani na kuendelezwa shuleni, akitaka ushirikiano wa karibu kati ya wazazi na walimu. Alisema katika enzi hizi za kidijitali, jukumu la mwalimu limebadilika; sio tena mfundishaji pekee, bali ni mwezeshaji anayemwongoza mwanafunzi kutumia teknolojia kujifunza kwa usalama na ufanisi.
"Ninyi walimu ni chachu ya mabadiliko na moyo wa mfumo wetu wa elimu. Mnatakiwa kuwaongoza wanafunzi wetu kuwa raia bora wa kidijitali," alisema Kazenga. Aliongeza kuwa serikali inaendelea na jitihada za kuboresha mitaala na kuingiza matumizi ya TEHAMA katika elimu ili kuhakikisha watoto wanapata maarifa stahiki.
Kwa upande wake, shirika lisilo la kiserikali la Room to Read, kupitia kwa Mkurugenzi Mkaazi wake, Joan Minja, lilieleza jinsi linavyochangia katika kuimarisha stadi za Kusoma, Kuandika, na Kuhesabu (KKK). Minja alibainisha kuwa tangu kuanza kazi nchini mwaka 2012, shirika lake limesambaza zaidi ya vitabu milioni 1.4 vya hadithi vilivyoandikwa na waandishi wa Kitanzania na kuthibitishwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).
"Tunaamini maktaba ni sehemu muhimu ya kujenga stadi za msingi na kuimarisha tabia ya kusoma. Tumeshafikia halmashauri nyingi nchini, zikiwemo Temeke, Ubungo, Mvomero, Bagamoyo na Tanga Jiji," alifafanua Minja. Juhudi hizi za pamoja kati ya serikali na wadau ni muhimu katika kuhakikisha kizazi kijacho cha Tanzania kinakuwa na uwezo wa kushindana katika ulimwengu wa kidijitali.