Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Amani, Watanzania wamehimizwa kuendelea kuwa walinzi wa amani iliyopo nchini, wakitambua kuwa ndiyo uti wa mgongo wa maendeleo yote ya kijamii na kiuchumi. Wito huo umetolewa na Umoja wa Mataifa (UN) na wadau wengine, wakisisitiza kuwa amani si zawadi, bali ni tunu inayohitaji kulindwa kila siku.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Umoja wa Mataifa nchini, Nafisa Didi, alisema ingawa Tanzania inafurahia hali ya utulivu, jukumu la kila raia ni kuhakikisha hali hiyo inadumu. Alisema amani ndiyo kila kitu na bila hiyo, mipango ya maendeleo haiwezi kufanikiwa.
"Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhakikisha analinda amani tuliyonayo ili iendelee kuwa nguzo imara ya taifa letu," alisisitiza Didi. Alitangaza kuwa kilele cha maadhimisho hayo kitaifa kitafanyika kesho, Septemba 19, 2025, jijini Dodoma, chini ya kauli mbiu "Chukua Hatua Sasa, Ulinda Amani," ikiwa ni utangulizi wa siku rasmi ya kimataifa ambayo ni Septemba 21.
Kama sehemu ya vitendo vya kulinda amani, Didi alibainisha kuwa tayari vijana 1,500 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, na Dodoma wamepatiwa mafunzo maalum kuhusu umuhimu wa kuwa mabalozi wa amani katika jamii zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Global Peace Foundation Tanzania, Hussein Sengu, alitoa wito maalum kwa vyombo vya habari. Alivitaka viweke ajenda ya kudumu ya kuelimisha na kuhamasisha umma juu ya umuhimu wa amani. Akitoa mfano wa kusikitisha kutoka eneo la vita la Israel na Gaza, ambako zaidi ya waandishi wa habari 200 wamepoteza maisha wakitimiza wajibu wao, Sengu alisema ni funzo tosha la kuthamini na kulinda amani ya Tanzania kwa gharama zote.
"Matukio ya maeneo mengine duniani yanatukumbusha thamani ya amani tuliyonayo. Ni lazima tuilinde kwa wivu mkubwa," alisema Sengu.