Mashindano ya Vunjabei Cup 2025 yameandika historia mpya katika mkoa wa Iringa kwa kuweka zawadi kubwa ya Shilingi milioni 10 kwa mshindi wa kwanza. Zawadi hii kubwa imezidisha ushindani na kuongeza thamani ya mashindano ya ngazi ya chini ya mpira wa miguu, na kuleta hamasa mpya kwa wachezaji na mashabiki.
Kwa miaka mingi, mkoa wa Iringa umekuwa ukishuhudia mashindano ya soka katika ngazi za kata, ambapo zawadi za juu mara nyingi zilikuwa ndogo, kama vile mbuzi mwenye thamani ya takriban Shilingi 150,000, seti ya jezi, na mpira. Hali hii ilikuwa haichochei sana ushindani na maendeleo ya soka katika ngazi hizo.
Hata hivyo, mashindano kama Vunjabei Cup yana uwezo mkubwa wa kuinua hali ya michezo mkoani Iringa. Yanaweza kusaidia kuibua vipaji vipya vya soka, na kuwarudishia wananchi mapenzi yao kwa mchezo huo, ambao ulikuwa unaonekana kupungua. Hii ni pamoja na timu ya Lipuli FC, ambayo ilikuwa ikishiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, kushuka hadi daraja la tatu.
Michuano ya Vunjabei Cup sasa imeingia katika hatua ya pili na ya mwisho, ambapo timu 50 bora zilizofuzu kutoka ngazi ya awali zinashindana. Ngazi ya awali ilianza rasmi Januari 11, 2025.
"Katika hatua hii, tunazipa timu zote 50 vifaa maalum vya michezo ambavyo vitawasaidia katika safari yao ya kusaka ubingwa wa Vunjabei Cup 2025," alisema Mkurugenzi wa Vunjabei, Fredy Ngajilo.
"Tunatambua kuwa michezo sio burudani tu, bali pia ni afya na ajira. Tunaleta mashindano haya ili kuwapa vijana wetu fursa ya kuonyesha vipaji vyao na kujitengenezea maisha bora," aliongeza Ngajilo kwa furaha.
Kulingana na mkurugenzi huyo, bingwa wa Vunjabei Cup 2025 ataondoka na kitita cha Shilingi milioni 10, kiasi ambacho kimeongeza sana hamasa kwa wachezaji na mashabiki.
Uzinduzi wa hatua hii ya timu 50 bora ulikuwa na mchezo wa kusisimua kati ya Kalenga FC na Mgela FC katika uwanja wa Kalenga. Mchezo huo uliisha kwa sare ya 1-1.
Hadi filimbi ya mwisho, timu zote zilionyesha kiwango cha juu cha soka, zikithibitisha kuwa ushindani katika Vunjabei Cup 2025 umefikia viwango vya juu sana.
Mbali na mchezo mkali uwanjani, uzinduzi wa hatua ya makundi ulikuwa pia ni tamasha kubwa la burudani. Wasanii maarufu kama Stamina, Dulla Makabila, na Eze Nice waliwapagawisha mashabiki kwa nyimbo zao kali.
Stamina, akiwa na mashairi yake yenye nguvu, aliwahamasisha vijana kuhusu umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na kutumia vipaji vyao vizuri.
Dulla Makabila, kwa mtindo wake wa Singeli, aliwafanya mashabiki kusahau uchovu wa mechi na kuingia kwenye furaha ya kucheza, huku Eze Nice akihakikisha kuwa mashabiki wa Iringa wanajivunia burudani kutoka kwa msanii wao wa nyumbani.
Mratibu wa mashindano hayo, ambayo yanasimamiwa na Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Iringa, Fadhili Ngajilo, amesema kuwa ikiwa mashindano haya yatafanikiwa sana, kuna mpango wa kuyapanua hadi mikoa ya jirani.
"Tumeshuhudia mwitikio mkubwa kutoka kwa vijana na mashabiki wa soka. Ikiwa Vunjabei Cup 2025 itaendelea kufanikiwa kama hivi, tunapanga kuyaeneza hadi mikoa mingine ili kutoa nafasi kwa vipaji vipya zaidi kung'aa," alisema Fadhili Ngajilo.