Ousmane Dembélé, mshindi wa tuzo ya Ballon d'Or ya mwaka 2025, ameonyesha ukomavu wake baada ya kukosolewa vikali na baba wa mchezaji mwenzake, Lamine Yamal. Licha ya kwamba baba huyo alilalamika kuwa mwanawe alinyimwa tuzo hiyo, Dembélé ametoa kauli nzuri na ya hekima kwa mchezaji huyo chipukizi.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uhispania, ikiwemo El Chiringuito, baba wa Yamal, Mounir Nasrallah, alikosoa vikali matokeo ya kura za Ballon d'Or, akidai kuwa mwanawe ndiye aliyestahili kushinda. Nasrallah aliita ushindi wa Dembélé "aibu ya kimaadili," akisema, "Mwanangu bila shaka ni mchezaji bora duniani na anaweza kuleta tofauti kubwa kwenye mchezo. Hakuna mtu anayeweza kushindana na Yamal. Ni jambo la kushangaza kwamba hakushinda Ballon d'Or."
Dembélé na Yamal wote walikuwa na msimu mzuri mwaka 2024/2025. Dembélé aliongoza timu yake ya Paris Saint-Germain (PSG) kushinda mataji manne (treble), ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu. Alifunga mabao 35 na kutoa pasi za mwisho 16 katika mechi 53, na alitajwa kama Mchezaji Bora wa UCL na Ligi Kuu ya Ufaransa. Yamal naye alifanya vizuri, akifunga mabao 20 na kutoa pasi za mwisho 28 katika mechi 58 na aliisaidia Barcelona kushinda mataji matatu ya Uhispania. Hata hivyo, kutoshinda UCL kulimwacha nyuma kwenye kura za Ballon d'Or.
Licha ya ukosoaji huo mkali, Dembélé alijibu kwa utulivu. Katika mahojiano na gazeti la Mundo Deportivo, alisema, "Yamal ana ujuzi na ukomavu mkubwa kwa umri wake. Ikiwa mambo yatakwenda vizuri, anaweza kushinda tuzo nyingi za Ballon d'Or katika siku zijazo." Alimaliza kwa kusema, "Ninafuraha sana kushindana na wachezaji wengi wenye vipaji vya hali ya juu, wakiwemo Yamal."