Baba wa nyota chipukizi wa Barcelona, Lamine Yamal, ametangaza kutoridhika kwake na matokeo ya tuzo ya Ballon d'Or baada ya mwanawe kushindwa na mshambuliaji wa PSG, Ousmane Dembélé. Yamal alishika nafasi ya pili kwenye tuzo hizo.
Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Hispania, El Chiringuito TV, baba wa Yamal, Mounir Nasrallah, alisema, "Sitasema hii ni wizi, lakini nadhani ni aibu kubwa ya kimaadili iliyowahi kutokea. Sio kwa sababu ni mwanangu, lakini Lamine Yamal ni mchezaji bora duniani. Hawezi kushindanishwa na mtu yeyote."
Tuzo ya Ballon d'Or ya mwaka huu ilichukuliwa na Dembélé, ambaye aliiongoza PSG kutwaa mataji matatu (Ligue 1, Kombe la Ufaransa, na Ligi ya Mabingwa Ulaya). Dembélé alifunga mabao 35 katika mechi 53 msimu wa 2024/2025.
Kwa upande mwingine, Lamine Yamal aliisaidia Barcelona kushinda mataji matatu: La Liga, Supercopa, na Copa del Rey. Hata hivyo, walitolewa katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Rais wa Barcelona, Joan Laporta, alisema, "Ushindi wa Ligi ya Mabingwa uliongeza uzito mkubwa katika uamuzi wa majaji." Aliongeza kuwa bado anaamini kuwa Yamal atashinda Ballon d'Or katika miaka ijayo.
Yamal mwenyewe alichukulia matokeo hayo kwa utulivu, akisema, "Lazima niendelee kufanya kazi kwa bidii ili nishinde tuzo nyingi zaidi katika siku zijazo. Matokeo haya yananipa motisha."
Mshindi wa tuzo ya Ballon d'Or huchaguliwa na waandishi wa habari za soka kutoka duniani kote. Kila mwandishi huchagua wachezaji watano bora kutoka kwa orodha ya wateule, na mchezaji anayepata alama nyingi zaidi ndiye anashinda.