Wakati dirisha la usajili likiendelea kupamba moto, Klabu ya Pamba Jiji kutoka Mwanza imeonyesha kuwa haina utani baada ya kuingia sokoni kwa kishindo, ikilenga kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu. Ishara ya kwanza ya dhamira yao thabiti ni hatua yao ya kumfuatilia hadi nchini kwake Ghana nyota wa zamani wa Wekundu wa Msimbazi, Nicolaus Gyan, na kuanza naye mazungumzo.
Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa viongozi wa Pamba Jiji wameanza mawasiliano na winga huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani. Kinachorahisisha dili hili ni ukweli kwamba Gyan ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Klabu ya Fountain Gate. Hii ina maana kuwa Pamba Jiji haitahitaji kulipa ada ya uhamisho, jambo linalowapa wepesi wa kumshawishi kwa maslahi binafsi.
Chanzo ndani ya klabu kimeeleza kuwa Pamba Jiji inathamini uwezo wa Gyan kubadilika uwanjani, kwani anaweza kucheza kama mshambuliaji, beki wa kulia, na winga. "Kumsajili Gyan ni kama kupata wachezaji watatu kwa gharama ya mmoja. Ana uzoefu na anaifahamu ligi yetu, ndiyo maana tumeamua kumfuata. Tunaamini mazungumzo yatakwenda vizuri," kilisema chanzo hicho.
Nguvu ya usajili ya Pamba Jiji haijaishia kwa Gyan pekee. Wanaonekana kuvuka mipaka ya nchi, kwani wanahusishwa pia na kiungo fundi kutoka Zambia, Larry Bwalya, ingawa kuna taarifa za mvutano baada ya klabu yake ya Napsa Stars kudai bado ana mkataba. Vilevile, wanamtolea macho beki kisiki na nahodha wa zamani wa TP Mazembe, Kabaso Chongo, anayekipiga Kabwe Warriors ya Zambia.
Orodha yao inajumuisha pia majina ya ndani kama John Mbise kutoka Geita Gold, pamoja na mshambuliaji hatari kutoka Nigeria, Umar Abba, anayechezea Bugesera FC ya nchini Rwanda.
Alipoulizwa kuhusu mbio hizi za usajili, Afisa Mtendaji Mkuu wa Pamba Jiji, Peter Juma Lehhet, alikiri kuwa mchakato unaendelea lakini hakutaka kutaja majina hadharani. "Ni kweli tumeanza harakati za kuimarisha kikosi. Tunazungumza na wachezaji wapya na pia tunajadiliana na wale wa zamani tunaotaka kuwabakiza. Mashabiki wetu watarajie mambo mazuri, na kila kitu kitawekwa wazi wakati ukifika," alisema Lehhet.