Kocha mpya wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi, ameanza kazi rasmi kwa kuweka kigingi kwa waajiri wake wa zamani, Yanga SC, katika harakati zao za kumsajili kiungo mkabaji mahiri, Mohamed Damaro Camara. Kocha huyo raia wa Argentina ameweka wazi kuwa anamhitaji mchezaji huyo M-Guinea katika mipango yake ya msimu ujao, hasa kwa ajili ya kampeni za Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Mabingwa wa nchi, Yanga, walikuwa wameelekeza rada zao kwa kiungo huyo shupavu baada ya kuonyesha kiwango cha kuvutia mno katika msimu uliopita. Uwezo wake ulijidhihirisha hasa katika mechi kubwa dhidi ya vigogo hao, ikiwemo fainali ya Kombe la FA visiwani Zanzibar na michezo mingine migumu ya ligi, ambapo alifanya kazi ya ziada katika eneo la kiungo.
Habari kutoka ndani ya klabu ya Singida zinaeleza kuwa mazungumzo kati ya Yanga na uongozi wa Singida kuhusu uhamisho wa Camara yalikuwa yamefikia hatua nzuri. Hata hivyo, ujio wa Gamondi umebadili upepo. Kocha huyo, ambaye anawafahamu vyema Yanga, amepiga breki ya ghafla kwenye dili hilo, akisema hawezi kuruhusu mchezaji muhimu kama Camara kuondoka kirahisi.
Inaelezwa kuwa Gamondi ameuambia uongozi kuwa yeye ndiye atakuwa na kauli ya mwisho kuhusu nani anabaki na nani anaondoka. Kwa upande wa Damaro, amesisitiza kuwa mchezaji huyo bado ana mkataba na ni sehemu muhimu ya jeshi analotaka kulijenga kwa ajili ya mashindano ya kimataifa. "Gamondi anamfahamu vizuri Camara, amemuona akicheza na anaamini atamsaidia sana. Amesema kupoteza mchezaji wa kaliba yake kutakuwa ni pigo kwa malengo ya timu," kilisema chanzo cha habari.
Sababu kubwa ya Gamondi kukubali kibarua cha Singida ni kuona kuwa timu hiyo ina wachezaji wenye vipaji ambao, akiongeza mbinu zake, wanaweza kuleta ushindani mkubwa ndani na nje ya nchi. Hivyo basi, hataki kikosi chake kibomolewe, bali anataka kufanya maboresho katika maeneo machache tu aliyoyaainisha, huku akilinda nyota wake muhimu.