Kocha anayefahamika kwa kauli zake za kijasiri na mbinu za ushindi, Miguel Gamondi, ametangaza rasmi kuirejesha falsafa yake ya "upambanaji" katika soka la Tanzania, safari hii akiwa na kikosi cha Singida Black Stars. Akizungumza jijini Dar es Salaam, kocha huyo wa zamani wa Yanga ameweka wazi kuwa anatumia michuano ya Kombe la Kagame kama maabara ya kutengeneza kikosi cha kutisha kitakachotoa upinzani mkali kwenye Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.
Gamondi amesisitiza kuwa mashindano ya Kombe la Kagame, yanayoshirikisha timu kutoka ukanda wa CECAFA, yamekuja wakati muafaka na yatampa fursa ya kukipima kikosi chake dhidi ya timu zenye viwango tofauti. "Mimi ni mpambanaji na napenda ushindani. Kwa hiyo, tutayatumia mashindano haya kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho. Ninatengeneza timu ambayo haitaogopa mpinzani yeyote na itakuwa na uwezo wa kushinda kila mechi, hasa zile ngumu ambazo nazifurahia zaidi," alitamba Gamondi.
Hata hivyo, kocha huyo raia wa Argentina aliongeza kuwa dhamira yake si kupata ushindi pekee, bali kuhakikisha timu inacheza soka safi na la kuvutia ili kuwapa burudani mashabiki. Alifananisha soka na sanaa, akisema: "Mashabiki wanakuja uwanjani kutaka ushindi, lakini pia wanataka kufurahia mchezo. Ni kama mwanamuziki jukwaani, anawapa watu kile walichokuja kufuata na vitu vya ziada. Timu yangu itacheza soka la burudani."
Baada ya kuondoka Yanga mwaka 2024 na kujiunga kwa muda mfupi na Al Nasr Benghazi ya Libya, Gamondi sasa anakabiliwa na mtihani wake wa kwanza wa kimataifa na Singida Black Stars dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda katika mechi za Kombe la Shirikisho Afrika, watakaposafiri kuwafuata Septemba 20 kabla ya kurudiana nyumbani Septemba 26.
Kibarua chake kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kitaanza rasmi Oktoba 30, mwaka huu, watakapokuwa wageni wa Azam FC katika Uwanja wa Azam Complex, mechi ambayo itatoa picha ya awali ya ushindani anaouahidi.