Vita ya usajili kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga, imechukua sura mpya na ya kusisimua, ikikumbushia sakata la kiungo Yusuph Kagoma. Safari hii, mhusika mkuu ni kiungo mkabaji wa CS Sfaxien ya Tunisia, Balla Moussa Conte (21), ambaye amezua mkwamo wa kipekee: Klabu yake inataka ajiunge na Yanga, lakini yeye mwenyewe amegoma akitaka kutua Simba.
Habari za uhakika zinaeleza kuwa Yanga tayari imefikia makubaliano na klabu ya CS Sfaxien na inasemekana wamelipa ada ya uhamisho. Yanga sasa inasubiri Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC) itumwe ili mchezaji huyo ajiunge na kambi ya maandalizi ya msimu mpya.
Hata hivyo, mchezaji mwenyewe, Balla Moussa Conte, ameweka ngumu. Inadaiwa amekataa katakata kujiunga na Yanga, akisema hakushirikishwa katika makubaliano hayo na moyo wake upo tayari kuitumikia Simba. "Taarifa za sasa ziko hivi, Yanga walilipa fedha kwa CS Sfaxien, lakini mchezaji amekataa. Yeye anataka kuchezea Simba. Kwa hiyo mpaka sasa ITC haijatoka," kilisema chanzo chetu cha habari.
Inaelezwa kuwa kivutio kikuu cha Conte kwenda Simba ni mazungumzo ya moja kwa moja aliyofanya na Kocha Mkuu, Fadlu Davids. Kocha Fadlu, aliyevutiwa na kiwango cha Conte walipokutana kwenye mechi za Kombe la Shirikisho, amemhakikishia nafasi kwenye kikosi cha kwanza. Zaidi ya hapo, kiungo mwingine wa Simba raia wa Guinea, Moussa Camara, amekuwa akimpa maelezo mazuri kuhusu maisha ndani ya klabu hiyo, jambo lililomvutia zaidi Conte.
Sakata hili lilianza kimya kimya, ambapo Simba ilipeleka ofa ya kwanza kwa CS Sfaxien. Yanga wakaingilia kati na kutoa ofa kubwa zaidi. Simba wakarudi na kupandisha dau, lakini Yanga nao wakarejea na dau nono zaidi ambalo lilifanya klabu ya CS Sfaxien ikubali kumuuza kwao. Tatizo ni kwamba, walifanya makubaliano na klabu bila kupata ridhaa ya mchezaji.
Mvutano huu umeibua tena vita ya maneno kati ya wasemaji wa klabu hizo. Hivi karibuni, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alidokeza kuwa wamewazidi kete watani zao kwa mchezaji mmoja kutokana na wepesi wao wa kufanya maamuzi. Kwa upande wake, Meneja wa Habari wa Simba, Ahmed Ally, amewataka mashabiki kupuuza maneno ya mitandaoni, akisisitiza kuwa usajili wao unafanywa kwa "umakini wa ICU" na hawajamkosa mchezaji yeyote waliyemlenga.
Sasa, dunia ya soka la Tanzania inasubiri kuona wapi mzozo huu utaishia: Je, nguvu ya fedha ya Yanga kwa klabu itashinda, au mvuto wa Simba kwa mchezaji utaibuka kidedea?