Kocha Mkuu wa klabu ya Simba, Fadlu Davids, amefichua mikakati yake yote atakayoitumia katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF dhidi ya Al Masry. Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa leo saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania kwenye uwanja wa New Suez, nchini Misri.
Davids amesema kuwa yeye na wachezaji wake hawana wasiwasi wowote kuelekea mchezo huo muhimu. Ameweka wazi kuwa anataka kumiliki mchezo kama walivyofanya kwenye mechi mbili za hatua ya makundi dhidi ya CS Constantine ya Algeria na Bravo do Maquis ya Angola.
"Nakumbuka mechi mbili tulizocheza ugenini kwenye hatua ya makundi, tulipoteza moja na kutoa sare nyingine. Lakini ukiangalia, tulimiliki mpira na kucheza vizuri nje ya uwanja wetu wa nyumbani. Tulishambulia sana na kupiga mashuti mengi. Nataka tufanye hivyo tena kwenye mchezo huu. Timu hii inazidi kuimarika kila siku, na sasa tumeingia kwenye hatua kubwa zaidi. Tunahitaji kuonyesha uwezo wetu na kile tunachotakiwa kufanya," alisema Davids.
Aliongeza kuwa lengo lao ni kuwanyima wapinzani wao nafasi ya kuwashambulia kwa muda mrefu, na pia kupata mabao katika mchezo huo wa ugenini. Mabao hayo yatawapa faida kubwa katika mchezo wa marudiano utakaochezwa nyumbani Jumapili ijayo.
"Lengo letu ni lile lile ambalo nimekuwa nikisema mara kwa mara: kufunga bao moja au zaidi kwenye mchezo huu. Hilo ndilo lengo letu kuu. Ni muhimu sana kwenye michuano hii ya mtoano. Hata kama utashinda, sare au kufungwa, unaweza kusonga mbele kwa faida ya bao au mabao ya ugenini. Bila shaka, tutajaribu kulinda lango letu, lakini kupata bao ni muhimu sana," alisisitiza Davids.
Akizungumzia wapinzani wao, Al Masry, Davids alisema ni timu nzuri yenye wachezaji wenye uwezo mkubwa. Alisema amewaelekeza wachezaji wake jinsi ya kukabiliana nao.
"Al Masry ni timu nzuri sana, yenye kiwango cha juu. Wachezaji wao wengi wana uwezo mkubwa. Wanacheza na mabeki watatu nyuma na wanapenda kushambulia sana. Kwa hiyo, tutalazimika kuwanyima nafasi, lakini pia na sisi kuwashambulia tutakapopata mpira," alisema.
Davids alieleza kuwa kipa wake namba moja, Moussa Camara, anaendelea na mazoezi kama kawaida na yuko fiti. Hata hivyo, alisema hawezi kusema lolote kuhusu nani ataanza hadi atakapopata taarifa kutoka kwa kocha wa makipa kuhusu kipa atakayekuwa fiti kwa asilimia 100.
Ikumbukwe kuwa Camara hajaichezea Simba tangu alipoumia kwenye mechi dhidi ya Azam FC iliyochezwa Februari 24 mwaka huu.
Kocha huyo alisema kuwa amefurahishwa na timu yake kufika mapema nchini Misri na kuzoea hali ya hewa, ambayo haitawapa shida katika mchezo wa leo.