Wekundu wa Msimbazi, Simba SC, wanashuka dimbani kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa wakiwa na kifua mbele, tayari kuwakabili Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Klabu hiyo inaingia kwenye mtanange huu ikiwa na morali ya juu inayotokana na mafanikio ya hivi karibuni, ikiwemo ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate na, muhimu zaidi, kutinga hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuiondosha Gaborone United ya Botswana.
Akizungumza na wanahabari, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Seleman Matola, alikiri kuwa kikosi chake kipo tayari kwa vita ya alama tatu. Huku akionyesha heshima kwa benchi la ufundi la Namungo, Matola alisisitiza kuwa wamejipanga vya kutosha kuhakikisha ushindi unapatikana. "Hautakuwa mchezo mwepesi, tunawaheshimu wapinzani wetu, lakini lengo letu ni moja tu: alama tatu," alisema Matola. Aliongeza kuwa mara baada ya mchezo wa kimataifa, walianza mara moja maandalizi na amekuwa akinoa zaidi safu ya ushambuliaji ili kuhakikisha kila nafasi inayotengenezwa inazaa matunda. Hata hivyo, Simba itawakosa nyota wake wawili, Mohamed Bajaber na Abdul Razack, ambao ni majeruhi wa muda mrefu.
Kwa upande wa wachezaji, Antony Mligo alithibitisha kuwa wapo tayari kuendeleza wimbi la ushindi. "Sisi kama wachezaji tumejiandaa vizuri. Tunajua utakuwa mchezo mgumu, lakini tuko tayari kwa ushindani mkali," alisema Mligo.
Kutoka kambi ya Namungo FC, Kocha Mkuu Juma Mgunda, alisema wamejiandaa vilivyo kukabiliana na Simba, wakitambua ubora na kasi ya wapinzani wao. "Tunafahamu Simba wanatoka kwenye mashindano ya kimataifa na wana ari kubwa, lakini hilo halitutishi. Tutapambana kwa nguvu zote ili kuwapa burudani mashabiki wetu na kupata matokeo mazuri," alieleza Mgunda. Kauli yake iliungwa mkono na mchezaji Abdala Mfuko, aliyeahidi kuwa watafuata maelekezo ya mwalimu ili kuondoka na matokeo chanya.