Klabu ya Simba SC imeendeleza ubabe wake katika soka ya Afrika kwa kuweka rekodi ya kihistoria ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL) kwa mara ya sita katika historia ya klabu hiyo. Mafanikio haya yamepatikana baada ya kuwaondoa wapinzani wao, Nsingizini Hotspur ya Eswatini, katika mchezo wa marudiano uliochezwa jana jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo wa raundi ya kwanza ya marudiano, Simba ilipata sare tasa (0-0) dhidi ya Nsingizini, na hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-0, yaliyopatikana katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa nchini Eswatini Jumapili iliyopita. Rekodi za Simba katika misimu iliyopita zinasomeka: ilifuzu makundi mwaka 2003 na kuishia hapo, kisha misimu ya 2018/19, 2020/21, 2022/23 na 2023/24 yote ilifika hatua ya robo fainali.
Wageni, Nsingizini Hotspur, wakijua wana kazi kubwa ya kufuta deni la mabao manne, walianza mchezo kwa kasi kubwa. Katika dakika za mwanzo, walifanya mashambulizi mawili hatari. Katika dakika ya kwanza tu, mshambuliaji wao kutoka Uganda, Joel Madondo, nusura aipe timu yake bao la mapema baada ya kupenyezewa mpira mrefu, lakini beki imara Rushine De Reuck alifika haraka na kuokoa hatari hiyo. Mashambulizi yalirudiwa dakika ya sita ambapo Neliswa Dlamini alipiga shuti kali lililopanguliwa na kipa Yakoub Suleiman.
Kutokana na matokeo mazuri ya mchezo wa kwanza, wachezaji wa Simba walionekana kucheza bila shinikizo la kutaka kushambulia. Badala yake, walionekana kutaka kumiliki mpira na kupigiana pasi nyingi kwa lengo la kuvuta muda na kulinda ushindi wao wa ugenini.
Katika kipindi cha pili, wageni walirejea kwa kasi, wakitaka bao la mapema ili kuwarejesha mchezoni. Kwakhe Twala alipiga shuti kali dakika ya 60 lililookolewa na Yakoub, na baadaye mlinda mlango huyo wa Simba alijionea faulo ya Neliswa ikigonga mwamba wa juu na kurudi uwanjani. Kipa wa Nsingizini, Subusiso Dlamini, naye alifanya kazi ya ziada kwa kuokoa shuti kali la Elie Mpanzu.
Mwishoni mwa mchezo, nusura Simba ipate bao la heshima, lakini shuti kali la Jonathan Sowah, aliyeingia kama mchezaji wa akiba, liligonga nguzo ya chini na kuokolewa, baada ya makosa ya kipa Dlamini. Mwisho wa yote, ushindi huo wa jumla unaipa Simba nafasi ya kuendelea kuota ndoto za kufika mbali zaidi msimu huu.