Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga Sports Club, wamefanikiwa kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kishindo baada ya kuicharaza Kagera Sugar mabao 4-0. Mchezo huo ulipigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, uliopo jijini Dar es Salaam. Ushindi huo wa jana umeongeza pointi za Yanga hadi kufikia 42 baada ya kucheza michezo 16. Katika msimu huu, Yanga imeshinda michezo 14 na kupoteza miwili, huku ikiwa haijatoka sare hata mara moja.
Hata hivyo, furaha ya Yanga kukaa kileleni inaweza kuwa ya muda mfupi, kwani hatima yao itajulikana leo. Simba Sports Club itakuwa ugenini kupambana na Tabora United kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, uliopo Tabora. Ikiwa Simba itashinda mchezo huo, Yanga itashuka hadi nafasi ya pili. Lakini endapo Simba itatoka sare au itapoteza, basi Yanga itaendelea kujivunia kilele cha ligi.
Mchezo ulianza kwa kasi huku Yanga wakionyesha nia ya kutaka kupata bao la mapema. Tayari katika dakika ya pili, Mudathir Yahya aliunyakua mpira kutoka kwa mabeki wa Kagera Sugar na kumtengea pasi safi Stephane Aziz Ki, ambaye alipiga shuti lililopaa juu kidogo ya lango la Kagera.
Mashambulizi ya Yanga hayakuishia hapo. Dakika ya 15, Aziz Ki aliwazidi ujanja mabeki wa Kagera na kumpasia Clement Mzize, lakini shuti lake liliishia nje ya goli. Baada ya muda ambapo mabeki wa Kagera Sugar walikuwa bize kuzima hatari zinazoelekezwa langoni mwao, ngome yao ilididimia katika dakika ya 31. Clement Mzize aliifungia Yanga bao la kwanza baada ya kupokea pasi murua kutoka kwa Aziz Ki, kufuatia makosa ya mabeki wa Kagera waliocheza mpira kwa uzembe. Bao hilo lilikuwa la saba kwa Mzize katika msimu huu.
Dakika ya 35, Yanga ilipata penalti baada ya Hijja Shamte kumfanyia madhambi Mudathir Yahya ndani ya eneo la hatari. Hata hivyo, kipa wa Kagera, Ramadhani Chalamanda, aliweza kuokoa mkwaju wa penalti wa Aziz Ki. Lakini bahati haikuishia hapo kwa Kagera, kwani mpira uliorejea ulifika kwa Israel Mwenda, ambaye alipiga shuti lililokwenda nje.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuongeza kasi zaidi. Mudathir Yahya aliandika bao la pili katika dakika ya 59, akimalizia kwa ustadi krosi safi iliyochongwa na Prince Dube.
Dakika ya 77, Pacome Zouzoua aliifungia Yanga bao la tatu kupitia penalti. Penalti hiyo ilitolewa baada ya Maxi Nzengeli kuangushwa ndani ya eneo la hatari. Mwamuzi Nassor Mwinchui hakusita kuashiria penalti kwa mara ya pili katika mchezo huo.
Yanga ilikamilisha karamu yao ya mabao katika dakika ya 85 kupitia kwa Kennedy Musonda. Bao hilo la nne lilifungwa baada ya kona fupi iliyochezewa na wachezaji kadhaa kabla ya mpira kumfikia Musonda. Alitumia vizuri makosa ya mabeki wa Kagera na kipa wao Chalamanda, ambao walionekana kutoelewana ni nani aangalie mpira.
Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 42, na sasa inasubiri kwa hamu matokeo ya mchezo wa Simba dhidi ya Tabora United. Kwa upande mwingine, Kagera Sugar inabaki na pointi 11 na inashika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi, hali inayoifanya kuwa katika hatari kubwa ya kushuka daraja.
Yanga inaendelea kuonyesha ubora wake msimu huu, na mashabiki wao wana matumaini makubwa ya kuiona timu yao ikitetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.