Simba Day 2025: Kishindo Cha Burudani na Nyota 13 Wapya Chatinga Mkapa

sports | Thu Sep 11 2025


Simba Day 2025: Kishindo Cha Burudani na Nyota 13 Wapya Chatinga Mkapa

Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam jana ulifurika na kugeuka kuwa bahari ya rangi nyekundu na nyeupe, huku maelfu ya mashabiki wa Klabu ya Simba wakishuhudia kilele cha tamasha lao la kila mwaka, maarufu kama 'Simba Day'. Tukio hili la 17 tangu kuanzishwa kwake lilikuwa mahususi kwa ajili ya kuzindua kikosi kipya cha msimu wa 2025/26, likiwa limepambwa kwa burudani kabambe na shamrashamra za aina yake.


Vumbi lilitimka mapema uwanjani hapo wakati wasanii wakubwa wa muziki nchini walipopanda jukwaani. Msanii Chino Wanaman aliziamsha hisia za Wanasimba kwa vibao vyake vikali kama ‘Yesa’ (Funga Mageti) na ‘Gibela remix’, vilivyomfanya kila shabiki aliyekuwa ameketi ashindwe kujizuia na kunyanyuka kucheza. Burudani ilifikia kilele pale msanii Mbosso alipoingia kwa mbwembwe na kutoa burudani ya kiwango cha juu kupitia nyimbo zake kama 'Selemani', 'Athumani', na 'Pawa', huku umati mzima ukiimba naye sambamba. Mwanadada Dj Sinyorita na bendi kongwe ya African Stars 'Twanga Pepeta' nao hawakuwa nyuma katika kuhakikisha shangwe halitulii.


Mbali na burudani, tukio hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo mgeni rasmi Waziri wa Maji, Jumaa Aweso. Mwekezaji na Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohamed 'Mo' Dewji, pamoja na uongozi mpya wa Bodi ya Wakurugenzi wakiongozwa na Mwenyekiti Crescentius Magori na mjumbe mpya Barbara Gonzalez, walikuwepo kushuhudia tukio hili muhimu.


Baada ya burudani, ilifuata sehemu iliyosubiriwa kwa hamu na wengi: utambulisho wa kikosi cha msimu mpya. Kazi hiyo ilifanywa na Meneja wa Habari, Ahmed Ally, ambaye alianza na benchi la ufundi kabla ya kuwaita wachezaji mmoja baada ya mwingine.


Simba imekisuka upya kikosi chake kwa kuwaongeza wachezaji wapya 13. Kati yao, saba ni wazawa: Selemani Mwalimu (kutoka Wydad Casablanca), Wilson Nangu na Yakoub Suleiman (wote kutoka JKT Tanzania), Mourice Abraham (kutoka RFK Novi Sad, Serbia), Antony Mligo (kutoka Namungo), Vedastus Masinde (kutoka TMA), na Charles Daud Semfuko (kutoka Coastal Union).


Orodha ya wachezaji wa kimataifa ina majina sita mapya: Jonathan Sowah (Ghana, kutoka Singida Black Stars), Mohamed Bajaber (Kenya, kutoka Polisi Kenya), Rushine De Reuck na Neo Maema (wote Afrika Kusini, kutoka Mamelodi Sundowns), Allasane Kante (Senegal, kutoka CA Bizertin), na Naby Camara (Guinea, kutoka Al Waab FC).


Wachezaji 12 wa zamani wamebaki kikosini, wakiwemo Shomari Kapombe, Mzamiru Yassin, Kibu Denis, na Moussa Camara. Hata hivyo, klabu imewaacha wachezaji kama Edwin Balua, Fondoh Che Malone na Leonel Ateba, huku wengine kama Salehe Karabaka na Velentino Mashaka wakitolewa kwa mkopo kwenda JKT Tanzania. Siku ilihitimishwa kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Gor Mahia kutoka nchini Kenya.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.