Winga wa klabu ya Arsenal FC, Bukayo Saka mwenye umri wa miaka 23, ameonesha wazi mapenzi yake kwa timu hiyo ya London Kaskazini. Kauli yake inakuja wakati timu yake ikijiandaa kwa mchezo mkubwa wa robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya (UEFA) dhidi ya Real Madrid. Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa leo saa nne usiku (saa 11:00 kwa saa za Uingereza) katika uwanja wa Emirates.
Saka, aliyezaliwa mwaka 2001, amekuwa mchezaji muhimu sana chini ya kocha Mikel Arteta katika kikosi cha Arsenal. Katika msimu huu pekee, ameshaonekana katika michezo 26 ya mashindano yote, akifanikiwa kufunga mabao 10 na kutoa pasi za mabao 14. Licha ya kuwa amebakiza miaka miwili katika mkataba wake na Arsenal, kumekuwa na uvumi kuhusu uhamisho wake. Hata hivyo, katika mkutano na waandishi wa habari jana kuelekea mchezo dhidi ya Real Madrid, Saka alikanusha uvumi huo.
"Nina amani kabisa kwa sababu nimebakiza miaka miwili kwenye mkataba wangu. Kila mtu anajua ninachofikiria. Nimekwishawaambia ninyi pia, kwa hivyo sihitaji kuharakisha," alisema Saka kwa ujasiri.
Aliendelea kueleza: "Ninatamani kushinda nikiwa nimevalia nembo ya Arsenal. Ninaipenda klabu hii na mashabiki wake, na nadhani mashabiki na klabu pia wananipenda. Ni uhusiano mzuri. Nina furaha sana kuichezea Arsenal na nimejikita kikamilifu katika kuhakikisha tunapata ushindi."
Saka aliongeza umuhimu wa mchezo wa leo kwa kusema: "Hii itakuwa usiku muhimu sana kwetu katika hatua ya robo fainali. Tunacheza dhidi ya moja ya timu bora katika mashindano haya, kwa hivyo tunahitaji kucheza vizuri. Ni mara ya kwanza kwa klabu kufika hatua hii ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa mfululizo. Kwa hivyo, tunataka kwenda hatua inayofuata kesho usiku na kuvuka mstari wa kumalizia."
Mchezo huu unakuwa mara ya tatu kwa Arsenal na Real Madrid kukutana katika mashindano ya Ulaya. Mara ya mwisho walikutana ilikuwa katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2005-2006. Katika mchezo wa kwanza uliochezwa ugenini, Arsenal walishinda 1-0 kwa bao la Thierry Henry, na mchezo wa pili walitoka sare ya 0-0. Katika msimu huo, Arsenal walifika fainali, ambayo ilikuwa mafanikio yao makubwa zaidi katika historia ya klabu kwenye Ligi ya Mabingwa. Mashabiki wa Arsenal nchini Tanzania na duniani kote wana matumaini kuwa Saka na wenzake wanaweza kuandika historia nyingine leo usiku.